Muigizaji na muongozaji wa filamu Tanzania Jacob Steven maarufu kama JB, amesema mwaka 2017 hakuwa mzuri kwa wasanii wa tasnia hiyo, kwani soko la filamu kwao lilikuwa la kusuasua.
Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, JB amesema tasnia ya filamu inakumbwa na tatizo kubwa la usambazaji wa kazi zao, kitendo ambacho wafanyabiashara wa filamu wanahofia kuwekeza pesa ya kutosha kwenye tasnia hiyo.
“Mwaka 2017 hakuwa mzuri kwa bongo movie, tumekuwa na tatizo kubwa sana la usambazaji, usambazaji ni tatizo kubwa sana, kwa sababu hawa watayarishaji ni wafanya bisahara pia, hawezi kuweka pesa zake kama haoni ni namna gani pesa zake zinaweza kurudi, hivyo tulikuwa tunasua sua lakini ujio wa barazani umesaidia sana, na nawaahidi mwaka 2018 tutafanya makubwa sana”, amesema JB.
Pamoja na hayo JB amekiri kuwa ubora wa filamu nao ni moja ya sababu ambazo zinafanya soko hilo kutofanya vizuri, jamboa ambalo pia amesema limefanyiwa kazi kwani kufikia mwakani hakuna filamu ambayo itashutiwa kwa camera za kawaida zaidi ya kutumika kwa red camera.