Baraza la Ushauri la Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra CCC) limewataka watumiaji wa huduma za usafiri kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapokutana na ongezeko la nauli katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dk, Oscar Kikoyo amesema tayari ameshaanza kusikia malalamiko ya upandishwaji wa nauli unaofanywa kinyemela na baadhi ya watoa huduma za usafiri na hatua zimeanza kuchukuliwa dhidi yao.
Amesema changamoto kubwa inayojitokeza ni watumiaji wa huduma hizo kuwa wazito kutoa taarifa wanapokutana na mambo yasiyofaa ikiwemo kupandishiwa nauli, mwendo kasi kwa kuhofia uhakika wa safari zao.
“Kuna kitu tunatakiwa tubadilike watanzania, yaani utakuta mtu anatozwa nauli kubwa na akiingia kwenye basi mwendo wa dereva unakuwa sio mzuri lakini hakuna anayesema. Wakati mwingine watu wa usalama barabarani wanaingia kwenye mabasi kuhoji lakini hakuna anayepaza sauti wanaishia kunung’unika,
“Tunaomba mtoe taarifa, nauli hazijapanda na usafiri upo wa kutosha ila kuna watu wachache wasio na nia njema wanataka kutumia mwanya wa kuwepo abiria wengi kutengeneza uhaba. Hakuna mmiliki wa chombo cha usafiri anayeruhusiwa kupandisha nauli kwa sababu abiria wapo wengi ,ukiona mtu anakutajia bei tofauti jitahidi hata umrekodi ili ashughulikiwe,” amesema
Kauli hiyo ya Dk Kikoyo imekuja ikiwa tayari hali ya sintofahamu imeanza kujitokeza katika kituo cha mabasi ya mikoani ya Ubungo ambapo baadhi ya watoa huduma ya usafiri wameanza kupandisha nauli.
Sanjari na ongezeko hilo haramu la nauli kumekuwepo pia msongamano wa abiria wanaotaka kwenda mikoani kwa ajili ya sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.
Dk Kikoyo pia ametoa tahadhari kwa watoa huduma za usafiri kutoruhusu watu wanaopanda kwenye mabasi na kuhubiri dini na siasa.
Kando na hilo amesema abiria wasisite kutoa taarifa endapo nyimbo na video zitakazowekwa ndani ya basi zitakiuka maadili ya Kitanzania