Mkazi wa Mtaa wa Kilimahewa katika Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara, Paul Juma (38), ameuawa kwa kuchomwa mshale na rafiki yake, baada ya kutokea ugomvi kati yao.
Inadaiwa ugomvi huo ulitokana na kumdai amuongeze Shilingi 4,000 kutokana na kumuuzia mabati manne chakavu kwa jumla ya Sh. 20,000.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Kamishna Msaidizi wa Polisi Jafari Mohamed, jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja mtuhumiwa kuwa ni Julius Mtoni (48) mkazi wa mjini Bunda na watu hao walikuwa ni marafiki.
Kamanda Mohamed alisema tukio hilo lilitokea Desema 26 majira ya mchana wakati watu hao walipokuwa wanakunywa pombe ya kienyeji kwa mwanamke ambaye ni jirani yao.
Polisi wilayani hapa walisema Desemba 25, marehemu alimuuzia mtuhumiwa mabati manne chakavu kwa makubaliano ya kila bati Sh. 7,000.
Walisema kuwa siku hiyo mtuhumiwa huyo alimpatia marehemu Sh. 20,000 taslimu na kukubaliana kuwa atalipwa kiasi kingine cha Shilingi 8,000 kilichobakia siku nyingine.
Walisema Desemba 26 wakiwa wanakunywa pombe, marehemu alimdai mtuhukiwa amlipe Sh. 8,000 zilizokuwa zimesalia, lakini alimpatia Sh. 4,000 ndipo wakaanza kuzozana huku marehemu akishinikiza alipwe deni lake lote la Sh. 8,000.
Aidha, ilielezwa kutokana na kutokuelewana, marehemu alianza kumkaba mtuhumiwa, kisha kukimbilia nyumbani kwake na kuchukua upinde na kumfyatulia mshale ambao ulimpata begani.
Polisi walisema kuwa baada ya marehemu kuchomwa mshale huo aliuvunja na kubakiza kipande cha mshale huo mwilini mwake na kukimbilia polisi, lakini alipoteza maisha kutokana na kutokwa na damu nyingi.
“Baada ya kuchomwa mshale huo marehemu aliuvunja na kubakiza kipande kikiwa mwilini mwake na kuja hapa polisi kisha hospitalini, lakini taarifa ya hospitali inaeleza alikufa baada ya kutokwa na damu nyingi,” alisema ofisa mmoja wa polisi ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake kwa madai sio msemaji wa jeshi hilo.