Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Singida inamshikilia mshindi wa kwanza kura za maoni CCM jimbo la Singida kaskazini, Haider Hussein Ghulamali (46), kwa tuhuma ya kutoa rushwa ya shilingi milioni mbili taslimu kwa afisa usalama wa taifa (jina tunalo).
Lengo la Ghulamali mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha magodoro mjini Dodoma,ni kwamba afisa usalama huyo amtolee taarifa nzuri Kwenye vikao vya ngazi za juu, ili aweze kuthibitishwa na vikao hivyo, kuwa mgombea ubunge jimbo la Singida kaskazini.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Joshua Msuya, alisema Ghulamali amekamatwa Desemba 12 mwaka huu saa 8.30 mchana, maeneo ya Rafiki resort wakati akikabidhi rushwa hiyo iliyokuwa imehifadhiwa kwenye bahasha.
Msuya alisema desemba 11 mwaka huu,ofisi yake ilipata taarifa ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwa mmoja wa wana CCM anayewania ubunge jimbo la Singida, ambaye ni Ghulamali.
“Baada ya kupokea taarifa hiyo uchunguzi ulianza ikiwa ni pamoja na kuchunguza vitendo rushwa alivyofanya mtuhumiwa huyo, kabla na baada ya kura za maoni kupigwa desemba 10 mwaka huu huko kijiji cha Ilongero.Kura hizo zilimpitisha Ghulamali aliyepata kura 606 kati ya kura 1009 zilizopigwa,” alisema.
Mkuu huyo, alisema baada ya zoezi hilo kupita la kura za maoni,mtuhumiwa kwa juhudi zake aliweza kupata namba za simu za afisa wa usalama wa taifa ambaye walikuwa hawafahamiani.
“Baada kupata namba ya simu ya afisa usalama taifa, Ghulamali aliweza kumpigia na akatoa maombi yake ya kusafishiwa taarifa kwenye vikao vya juu.Baada ya maombi hayo,aliweza kutoa rushwa ya shilingi milioni mbili,na kumkabidhi afisa huyo. Ndipo alipokamatwa na TAKUKURU waliokuwa wameweka mtengo,” alisema Msuya.
Alisema uchunguzi zaidi bado unaendelea kuhusiana na mtuhumiwa Ghulamali kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi wa kura za maoni.
Mkuu huyo wa TAKUKURU,ametoa rai kwa wanachama wa vyama vyote vya siasa,wagombea na wananchi kwa ujumla, kuzingatia sheria za uchaguzi ndani ya vyama vyao.Pia kujiepusha na vitendo vya rushwa nyakati za uchaguzi ndani vyama.
“TAKUKURU itamkamata mgombea,mpambe na mwanachama yeyote atakayejihusisha na vitendo ya kuomba na kupokea rushwa,na ikipata ushahidi wa kutosha,itamfikisha mhusika mahakamani,” alisema Msuya
hongera sana Mr president naielewa serikali yako sasa kamata yeyote walizoea zama zile na sasa zimeshapita
ReplyDeleteKabisa rushwa ni adui wa haki na huwezi kuhubiria watu kuacha maovu kabla ya kujisafisha wewe mwenyewe kwanza. Na kwa matukio yanayoendelea kutokea ndani ya chama cha mapinduzi ya watu kushikwa na rushwa inadhihirisha uthubutu na ujasiri wa hali ya juu wa muheshimiwa raisi Magufuli wa kupambana na rushwa. Kupambana na maovu yaliyokisiri katika maisha ya mtanzania. Rushwa ni rushwa hata kama ni kidogo. Haki na usawa kwa wote ni kitu kigumu kutekelezeka katika jamii lakini kukosekana kwa usimamizi wa haki ni chanzo cha matabaka katika jamii na ni mwanzo ya laana za M/MUNGU zinapoishukia jamii husika hasa ufukara na umasikini. Umasikini na ufukara hushamiri katika jamii iliyojaa dhambi za rushwa na kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa wana jamii. Nchi zote zilizopiga hatua duniani zilizingatia uadilifu wa watu wake kwa kuweka sheria kali na adhabu za mfano zidi ya vitendo vya rushwa hasa kwa watumishi wa umma bila ya kujali au kuoneana haya. Kazi anayoiendeleza Magufuli ni ya mfano na uungwaji mkono kwenye harakati za mapambano zidi ya rushwa unahitajika kwa nguvu isiokipimo kwa kila mtanzania mwenye kujitakia maendeleo na nchi kwa ujumla.
ReplyDelete