Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru ) , Valentino Mlowola amekanusha kuwa wametupilia mbali ushahidi wa Mbunge wa Arumetu Mashariki, Joshua Nassari na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema juu ya tuhuma za kununuliwa kwa baadhi ya madiwani katika Chama chao na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM ).
Akiongea na Bongo5 leo, Makao Makuu ya Taasisi hiyo, Mkurugenzi huyo amesema kuwa Taasisi hiyo ina mamlaka sheria ya kuchunguza tuhuma zote zinazohusiana na rushwa nchini.
“Taasisi hii kisheria ina mamlaka sheria ya kuchunguza tuhuma zote zinazohusiana na rushwa nchini na jukumu hilo linaendelea kufanywa kwa kufuata taratibu za kisheria kwahiyo uchunguzi wa tuhuma zote za rushwa unaendelea mpaka tunapo jidhihirisha kuwa kosa limefanyika au halijafanyika”
“Hakuna kitu kama hicho, uchunguzi madamu kama unahusu tuhuma za rushwa lazima unaendelea tu suala la kwamba tunatupilia mbali tumetupilia mbali nini utaratibu tukishamaliza uchunguzi tunapeleka jalada kwa Mwanasheria mkuu wa serikali ana tathimini ule ushahidi kutoka hapo anapendekeza au anachukua hatua anazopaswa kuchukua.”
Awali kulikuwa na taarifa zikienea kuwa, Taasisi hiyo imefuta jalada liliwasilishwa na wabunge hao kwa kile kilichodaiwa kuwa wamevuruga uchunguzi na kuweka kila kitu hadharani wakati bado taasisi hiyo ikiendelea na uchunguzi.