Tanzania inaongeza maradufu idadi ya panya buku wanaotumika kuutambua ugonjwa wa kifua kikuua.
Panya hao hupewa mafunzo na wana uwezo wa kunusa kamasi za binaadamu na kutambua kwa haraka ugonjwa wa TB.
Wana uwezo wa kutambua sampuli mia moja kwa muda usiozidi dakika 20.
Tofuati na binaadamu - wataalamu wa maabara wanaotumia siku nne kuchunguza idadi hiyo ya sampuli.
Tanzania sasa itawatumia panya hao katika kliniki zipatazo 60 kote nchini.
Mfumo huu wa kutumia panya kutambua TB ulianzishwa na shirika la misaada Ubelgiji, kama njia nyepesi na na isiyotumia fedha nyingi kutambua TB kinyume na mfumo uliozoeleka.
Katika baadhi ya mataifa kusini mwa jangwa la Sahara, zaidi ya 50% ya wagonjwa wa TB hawatambuliwi au hawatibiwi na kote duniani, idadi hii ni ya juu kiasi cha milioni 4.1.
Kutotambuliwa kwa wagonjwa hawa wanaojumuisha watu wasiojiweza, na wasioweza kupata matibabu - wazee kwa vijana, watu wanaoishi katika umaskini, wachimbaji migodi na hata wahamiaji.
Iwapo mgonjwa hatopata matibabu, mgonjwa TB anaweza kusambaza ugonjwa huo kwa hadi watu 15 kwa mwaka.
Tanzania ni mojawapo wa mataifa 30 ambako kunashuhudiwa maambukizi makubwa ya kifua kikuu, ambao ni ugonjwa mmojawapo hatari unaosambaa kwa kasi na kuua watu, lakini unaoweza kutibiwana kuzuiwa.