Tanzia: Tasnia ya Habari Yapata Pigo Mayage Amefariki Dunia.

Tanzia: Tasnia ya Habari Yapata Pigo Mayage Amefariki Dunia.
Mwandishi wa habari mwandamizi, Mayage S. Mayage amefariki dunia.

Mayage (56), amefariki dunia leo Jumapili Desemba 25,2017 katika Hospitali ya Misheni ya Mbweni jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa.

Emmanuel ambaye ni mdogo wake na Mayage katika taarifa amesema madaktari waligundua kaka yake alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya saratani na kifua kikuu.

“Mayage aligundulika kuwa na saratani mwaka mmoja uliopita na alipata matibabu katika hospitali mbalimbali nchini zikiwemo Ocean Road na Muhimbili,” amesema.

Amesema hali yake iliimarika kwa muda, lakini ikabadilika wiki tatu zilizopita na kusababisha kulazwa katika Hospitali ya Mbweni.

Emmanuel amesema Mayage atazikwa Alhamisi Desemba 28,2017 katika makaburi ya Mbweni eneo la Maputo.

Amesema utaratibu unaendelea kufanyika nyumbani kwa Mayage, Mbweni Kijijini eneo la Maputo ambako ndugu na jamaa wanakutana.

Mayage alianza kazi za uandishi wa habari mwaka 1995 katika kampuni ya Habari Corporation Ltd (HCL).

Baadaye alifanya kazi hiyo akiwa mwandishi wa kujitegemea akijiita “mwandishi huru” na alifanya kazi katika magazeti ya Raia Tanzania, MwanaHalisi na hadi kifo chake alikuwa akifanya kazi na gazeti la Tazama.

Salva Rweyemamu, aliyekuwa mhariri mtendaji wa magazeti ya HCL amemzungumzia Mayage akisema alikuwa mwandishi mzuri, mahiri, asiyeogopa na aliyefanya kazi kwa weledi.

Amesema alikuwa mchambuzi mzuri wa habari za siasa.

“Mayage hakushindwa kazi yoyote aliyotumwa, ukimwagiza lazima uwe na uhakika wa kuifanikisha, hakika tumepoteza mchapakazi,” amesema Salva.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad