Tetemeko Latokea Chamwino Mkoani Dodoma na Kuleta Madhara Katika Nyumba Zaidi ya 60

Tetemeko Latokea Chamwino Mkoani Dodoma
Wataalamu wa jiolojia wamesema kuwa tetemeko la ardhi limetokea Kata ya Aneti wilayani Chamwino usiku wa kuamkia jana lina ukubwa wa 5 katika kipimo cha richter.

Tetemeko lenye ukubwa wa 5.1 kipimo cha richter lilitokea Julai mwaka juzi katika kata hiyo na kusababisha nyumba zaidi ya 60 kupata nyufa.

Ofisa Mwandamizi wa Jiolojia katika Wakala wa Jiolojia Nchini (GST), Gabriel Mbogoni alisema tetemeko hilo limetokea katika maeneo lilipotokea mwaka jana Kusini

Mashariki wa mji wa Aneti.

Alipoulizwa kama tetemeko hilo lililotokea saa 9 limeleta madhara yoyote, Mbogoni alisema hajapata taarifa.

“Ukubwa wa 5 siyo la kawaida. Unakumbuka la Bukoba lilikuwa na ukubwa gani? Ni kama 5.7 tetemeko linaweza likawa na ukubwa wa tano hadi saba lakini lisilete madhara,” alisema.

Mbogoni alisema tetemeko linaweza likawa na ukubwa mdogo lakini likaleta madhara kutegemea na mpasuko wa miamba umetokea katika kina gani.

“Inategemea pia na eneo ambalo mawimbi yanapita, ile miamba iko namna gani,” alisema Mbogoni.

Alifafanua kuwa tetemeko hilo lilipiga kati ya sekunde nne na tano na kwamba likipiga kati ya sekunde 20 hadi 30 madhara yake ni makubwa sana.

Mbogoni alisema madhara hayo yanatokana na jengo kutikiswa kwa muda ambazo tetemeko linadumu.

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga alisema hadi jana mchana kulikuwa hakujaripotiwa madhara yoyote.

“Nimewasiliana na viongozi wa kule, diwani na mwenyekiti wa kitongoji wanasema ni kweli lilitokea lakini hadi sasa hakujaripotiwa madhara yoyote,” alisema.

Tetemeko kubwa la ardhi kutokea nchini lilitokea miaka tisa iliyopita katika eneo la Oldonyo Lengai ambalo lilikuwa na ukubwa wa 5.9 kwa kipimo cha richter.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad