Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga amelitaka jeshi la polisi nchini kufanya uchunguzi wake kwa haraka ili kuwezesha kupatikana kwa mwandishi wa habari wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Azory Gwanda.
Azory ametoweka siku ya 18 sasa huko Kibiti ambako anaishi na familia yake.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kufungua kongamano la maadhimisho ya siku ya haki za binadamu leo Ijumaa, Nyanduga amesema kupotea kwa mwandishi huyo kuna viashiria vya uvunjifu wa haki za binadamu.
"Matukio haya sasa yamekuwa mengi na yameanza kuzoeleka, tunaliomba jeshi la polisi lifanye uchunguzi wake haraka ili mwandishi huyu apatikane," amesema Nyanduga.
Amesisitiza kwamba kila mtu ana wajibu wa kulinda haki za binadamu lakini Serikali ndiyo ina wajibu mkubwa kwa sababu ina wajibu wa kulinda maisha ya watu wake.
Nyanduga amesema tume yake inalaani vitendo vyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu na mara nyingi wanaunda kamati kwa ajili ya kuchunguza matukio hayo na kutoa ripoti.