Ukarabati Wamkwamisha Rais wa Zimbabwe Kuingia Ikulu

Ukarabati Wamkwamisha Rais wa Zimbabwe Kuingia Ikulu
Rais wa Zimbabwe,  Emmerson Mnangagwa bado anaendelea kuishi nje ya ikulu akisubiri ukarabati ulioanza ili kurejesha katika hadhi yake.

Mnangagwa aliapishwa hivi karibuni kuwa Rais wa Zimbabwe akihitimisha miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe aliyeongoza taifa hilo tangu uhuru.

Hata hivyo, licha kuapishwa kiongozi huyo ameshindwa kuhamishia makazi yake katika ikulu ya taifa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ikulu hiyo kuhitaji matengenezo makubwa.

Kulingana na msemaji wa rais, George Charamba ikulu ya Zimbabwe ilitelekezwa kwa muda mrefu na Mugabe aliyehamishia makazi yake katika jengo lake ambalo anaendelea kuishi hadi sasa.

Amesema kutokana na kutokaliwa kwa muda mrefu hali ya ikulu hiyo siyo nzuri na hivyo kumfanya Mnangagwa ashindwe kuhamia. Ukarabati unaofanywa ni pamoja kupaka upya rangi jengo nzima na kuweka mifumo mingine inayotakiwa. Pia, imeelezwa kuwepo kwa matengenezo muhimu ya lazima.

Baadhi ya ripoti zinasema Rais Mnangagwa amekuwa akiendesha shughuli zake katika ofisi iliyokuwa ikitumiwa na makamu wa rais wa zamani, Joice Mujuru lakini hakuna maelezo yaliyotolewa sehemu anakoishi.

Wiki iliyopita, rais huyo alitangaza baraza lake jipya la mawaziri huku akiwajumuisha baadhi ya maofisa wa kijeshi. Hata hivyo, siku mbili baadaye aliwapangua baadhi ya mawaziri na kumweka kando waziri aliyekuwa akishughulikia elimu ambaye alilalamikiwa kuwa chanzo cha kushuka kiwango cha elimu nchini humo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad