Ibrahim Lauden (20), aliyekuwa mkazi wa Mtaa wa Makunguru jijini Mbeya aliugua saa chache tangu achukuliwe nyumbani kupelekwa Kituo Kikuu Polisi Mbeya na ingawa familia yake inahisi kifo chake baadaye kimetokana na kipigo, imekubali kuzika mwili huo baada ya awali kuususa ikitaka uchunguzi.
Mama mzazi wa Ibrahim, Ngetile Lauden, aliliambia Nipashe jana kuwa Ibrahim alilazwa katika Chumba Cha Wagonjwa Mahututi (ICU) kwenye Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya tangu Novemba 26 mpaka alipofikwa na umauti Jumamosi.
Alisema kikao cha wanafamilia kilichofikia maamuzi ya kuususa mwili huo kilifanyika juzi Mtaa wa Makunguru jijini hapa ambapo uamuzi huo uliungwa mkono na wakazi wengine wa mtaa huo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo ya mama mzazi wa marehemu huyo, jana wanafamilia walifanya kikao kingine na kuwaomba wakazi wenzao kubadili msimamo wa kutozika mwili huo ili usiharibike.Alisema wakazi hao waliridhia.
Akisimulia mkasa huo, Ngetile alisema Novemba 26 mwaka huu, saa 9:00 usiku, mwanawe alichukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa ni wanausalama wakidai ana makosa ambayo angeyajua akifika kituo cha polisi.
Alisema kutokana na kwamba walijitambulisha kuwa ni watu wa usalama, yeye na wanafamilia wengine hawakupata wasiwasi hivyo wakaendelea kusubiri kupambazuke ili waende kituoni kumuona na kuuliza sababu za kukamatwa kwake.
Ngetile alisema alijihimu akiwa ameongozana na dada zake kwenda Kituo Kikuu cha Polisi cha Mkoa wa Mbeya, wakiwa wamebeba chai, lakini walipofika mapokezi kwa ajili ya kuomba kumuona mwanaye huyo, waliambiwa anahojiwa hivyo hawaruhusiwi kumuona.
Alisema baada ya muda mfupi walimuona kijana wao huyo akiwa anapakiwa kwenye gari ya Polisi na kukimbizwa katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya, ndipo na wao wakaamua kwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kufuatialia kinachoendelea.
Alisema baada ya muda mfupi kijana huyo alirejeshwa tena kituoni lakini muda mfupi baadaye wakaamua kumrudisha tena hospitali na ndipo akapelekwa ICU.
“Walimchukua mwanangu akiwa mzima, hakuwahi kulalamika kichwa wala ugonjwa wowote, lakini alipofika huko sijui kilitokea nini akawa mahututi mpaka kufariki (baada ya kulazwa),” alisema Ngetile.
Mke wa marehemu, Sarafina Athuman, alisema wakati askari wakimchukua mumewe alikuwa haumwi na kwamba walipohoji sababu waliambiwa wawahi kituoni ndipo watakapojua sababu ya kukamatwa kwake.
KITUO KIDOGO
Sarafina alisema habari alizopata ni kuwa awali mume wake huyo hakupelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi na badala yake alipelekwa katika kituo kidogo cha Polisi Mwanjelwa.
Alisema asubuhi alipowahi kwenda kumuona alikuta yeye na wenzake wakitembea kuingia kwenye gari kwa ajili ya kupelekwa Kituo Kikuu.
Alisema mumewe alipopelekwa kwa mara ya pili hospitalini na kuingizwa ICU alitamka kuwa ‘anajisikia maumivu ya kichwa’ na baada ya hapo hakutamka kitu kingine kwa siku saba alizolazwa humo mpaka anafariki.Aidha, Sarafina alisema wakati anamwangalia mumewe akiwa ICU, alikuwa amevimba upande wa kushoto wa kifua, magoti na mikono.
“Mume wangu alikuwa hana tatizo lolote, lakini wakati yupo hospitalini kwenye chumba cha wagonjwa mahututi alitamka akisema ‘mimi kichwa’, basi,” alisema Sarafina. "Hakutamka kitu kingine."
Marehemu ameacha mjane huyo na mtoto mmoja wa kiume ambaye ana miezi 11.Naye mjomba wa marehemu, Ipyana Mwakitalima, alisema taarifa alizozipata ni kwamba Ibrahimu alipigwa wakati alipohoji sababu za kukamatwa kwake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alikiri kuwepo kwa tukio hilo na akasema tangu Ibrahim akamatwe alikuwa analalamika maumivu ya kichwa.
Aidha, Mpinga alidai kuwa walifanya uchunguzi na kubaini kuwa kijana huyo alikuwa mtumiaji wa dawa za kulevya na kwamba Jeshi hilo linasubiri taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha kifo chake kutoka kwa madaktari wa hospitali hiyo.
“Kwa mujibu wa sheria, mtuhumiwa anapokamatwa, hatakiwi kupigwa, lakini hutokea askari kutumia nguvu ya kiasi, inatokea mtu anaambiwa twende kituoni akakataa na huwezi kumwacha kwa sababu amekataa, hivyo tunafungua jalada la uchunguzi na kutafuta ushahidi,” alisema Kamanda Mpinga.
Alisema baada ya taarifa ya madaktari kutolewa, wataiweka wazi ili kila mtu ajuwe chanzo cha kifo cha kijana huyo.
Jamani polisi sometimes unapomkamata mtuhumiwa siyo alshabab huyo na hakuna mtu anaweza kuitwa polisi akakataa kuna vijisababu tu kama mtu kuuliza kosa lake tayari anatuhumiwa tena anakiburi kama polisi aliyepitia sheria za kukamata au utaratibu wa kumkamata mtuhumiwa anaweza kumjibu vile yeye anaona kulingana na uzito wa tuhuma siyo rungu hiyo kosa mtu akiuliza siyo kwamba amekataa
ReplyDelete