Mvutano umeibuka kati ya Jeshi la Uhamiaji mkoani Kilimanjaro na mchungaji wa kanisa la ‘Yesu Anaweza Centre’ Zakaria Yona pamoja na familia yake, kuhusu utata wa uraia wao.
Jeshi hilo lilimchukua mchungaji huyo na familia yake ya watu watano na kuwakabidhi Holili upande wa Kenya, lakini Serikali ya Kenya ikakataa kuwapokea.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, mchungaji huyo alisema licha ya Mahakama kutoa zuio la muda kwa jeshi hilo na mwanasheria mkuu wa Serikali, bado jeshi hilo linaendelea kuwabugudhi.
Mkuu wa uhamiaji mkoa wa Kilimanjaro, naibu kamishina wa uhamiaji (DCI), Albert Mwelamila alisema asingependa kuzungumzia malalamiko ya mchungaji huyo kwa vile ameshakwenda kortini.
“Ushahidi tuliokusanya unaonyesha si raia wa Tanzania na wamezaliwa Kenya sasa kwa sababu kuna zuio la Mahakama tunaheshimu hilo lakini tuna uhakika kuwa si raia wa Tanzania,” alisema Mwelamila.
Zuio la muda lililotokana na maombi namba 46/2017, lilitolewa Desemba 18 mwaka huu na Jaji Aishiel Sumari, ambaye aliwazuia wadaiwa kuwakamata wadai hadi shauri la msingi litakaposikilizwa.
Kwa mujibu wa amri hiyo, Jeshi la Uhamiaji na Mwanasheria mkuu wa Serikali, wamezuiwa kuwakamata mchungaji huyo na familia yake, ambayo ni pamoja na mkewe, Redempter Francis.
Hata hivyo, mchungaji huyo alidai kwamba siku moja baada ya kutolewa kwa zuio hilo, maofisa hao walikwenda nyumbani kwake eneo la Majengo kwa nia ya kuwakamata.