PAZIA ni miongoni mwa mapambo yanayotumika katika kupendezesha na kukoleza umaridadi wa ndani ya nyumba. Kama ilivyozoeleka, pazia zimekuwa zikitumika kupamba mlangoni na madirishani pia hasa maeneo ambayo chumba tunapoishi kinakosa faragha.
Lakini pia, katika sehemu zenye joto kali ambazo mara nyingi madirisha yake huwa na wavu au matobo, pazia imekuwa ikitumika wakati mwingine.
Halikadhalika, hata katika sehemu ambazo madirisha yake ni yale yasiyo na wavu, bado wanatumia pazia kama pambo la kupendezesha nyumba na miaka ya hivi karibuni limekuwa likitumika zaidi kuliko ilivyokuwa hapo zamani.
Na kwa sababu imezoeleka kwamba mwanamke ndiye anayesimamia mambo mengi nyumbani, pale inapokuwa haijapambwa na pazia ikapambika, huonekana kama hawajibiki ipasavyo katika majukumu yake kama mama na msimamizi wa uzuri na ubora wa makazi yake.
Mbali na nyumbani, pia pazia hutumika kupamba ofisi, hotelini na sehemu nyingine nyingi. Pazia za ofisini zinafahamika na zile za hotelini kwenye sehemu za vinywaji nako ziko za kupapendezesha.
Kadri ukuaji wa sayansi na teknolojia unavyochukua nafasi yake, kadhalika maisha nayo yanabadilika ama kuboreka zaidi huku huduma na bidhaa zikiboreshwa kila wakati.
Siku hizi tofauti na miaka ya nyuma, baadhi ya familia hupendelea hata wakati mwingine ndani ya nyumba kunapokuwa na pazia ng’aring’ari zenye mvuto, hulazimika kugharimia kuweka kiyoyozi ili pazia zisivurugike katika mpangilio na kuharibu muonekano mujarabu wa ndani wa nyumba kwa kisa tu kutafuta hewa.
Kwa ujumla pazia katika kipindi hiki cha kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia, zinatengenezwa katika aina au mitindo yenye mvuto tofauti na hivyo kutoa fursa kila mtu kuchagua aina inayomfaa hasa kwa kuzingatia mandhari iliyopo ndani ya nyumba yake.
Zipo pazia zilizotengenezwa kwa kutumia kitambaa kizito zaidi, za vitambaa vyepesi, hariri, zipo za turubai, shanga, fimbo za plastiki na hata za nyuzi.
Lakini pia zipo pazia ambazo zina matundu lakini zote kwa ujumla wake zimekuwa zikitumika kupamba nyumba, ofisi ama hoteli kulingana na mahitaji ama mandhari iliyopo katika sehemu husika.
Lakini pamoja na hayo uchaguzi wa rangi na aina ya kitambaa kwa wale wanaopendelea kushona, nalo ni jambo muhimu linalopaswa kuzingatiwa na wakati wa kufanya hayo yote kuzingatia aina ya rangi zilizopo katika nyumba unayoilenga kuanzia ukutani na vitu vingine vilivyomo ndani.
Kikubwa zaidi ambacho nimependa kuzungumzia pazia, ni kutokana na umuhimu wake katika kupendezesha makazi, ndiyo maana kuna umuhimu zaidi hasa kwa kina mama kuzingatia vigezo mbalimbali wanapofanya uchaguzi wa pazia hizo.
Ni vema kutambua kuwa ubaya wa nyumba yako utatokana na namna unavyoitengeneza na hata mvuto wake pia utatokana na namna unavyochagua na kupangilia wewe mwenyewe.
Ni jambo la aibu kuona unasifia mvuto wa nyumba ya jirani eti tu ameweka pazia nzuri, wakati na wewe mwenyewe unaweza.
Naamini kila kitu kinawezekana ukijipanga usitumie gharama kubwa katika kupata pazia bora unazozipenda kama utajipanga na kudhamiria kuwa nazo.
Wapo wanawake na wanaume ambao wanaweza kutundika pazia zao ndani ya nyumba kwa kutumia kamba za kawaida na ikapendeza lakini nashauri kama inawezekana si vibaya kutumia fimbo ama vibanio vya kutundikia pazia hizo vinavyouzwa madukani.
Fimbo hizi hupatikana kwa wingi katika maduka ambayo yanauza pazia kwa hiyo ni vema wakati unanunua pambo hilo ukatafuta na fimbo yake.
Ulizia fimbo au bomba ambazo rangi zake zinaendana na rangi iliyopo kwenye nyumba pamoja na iliyopo kwenye pazia. Mara nyingi bomba za kahawia, rangi ya maziwa na nyeusi isiyokolea hupendezesha.
Kwa kupata matokeo epuka rangi zinazong'ara kupindukia kwa sababu hazina utulivu, ni vema kuchagua rangi iliyopoa.
Zingatia kuweka pazia katika fimbo au bomba laini ambazo hazikwaruzi ili zisizisoharibu wakati unavuta kuziweka sawa ama unazitoa kuzifua ama kuondoa vumbi.
Zungumza na wataalamu wa urembo na mapambo ya nyumba ili kukupa ushauri zaidi. Suala la msingi ni kufahamu mbinu za uwekaji wa pazia. Kumbuka kuchanganya kama ni jepesi weka lenye lesi ndani.
Wakati mwingine ni vyema kubebesha pazi zito na lile la lesi ili joto linapozidi ulifungue mojawapo kupata hewa safi na mwanga.