Wafanyakazi Waliondolewa Kazini kwa Vyeti vya Dalasa la Saba Wadai Mafao Yao

Wafanyakazi Waliondolewa Kazini kwa Vyeti vya Dalasa la Saba Wadai Mafao Yao
Wafanyakazi 66 walioondolewa kazini katika Hospitali ya Rufaa KCMC mjini hapa, kutokana na kuwa na vyeti vya darasa la saba wamemtaka mwajiri kuwalipa mafao yao. Miongoni mwa waliositishiwa ajira ni aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Mhumba.

Pia, wamemtaka mwajiri kuwalipa mishahara ya miezi saba tangu waachishwe kazi mwezi Juni, wakidai utaratibu wa kuwaondoa haukufuatwa, hivyo wao bado ni wafanyakazi halali.

Mhumba alidai hawakuajiriwa na Serikali, bali KCMC ambayo alisema ina uwezo wa kuwalipa fedha kutokana na mapato yake.

Alidai KCMC inakwepa jukumu la kuwalipa na badala yake inasema inasubiri mwongozo kutoka serikalini.

Mhumba alisema hayo jana mbele ya msuluhushi na mwamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Mkoa wa Kilimanjaro, Godwin Migire.

Aliyekuwa mlinzi wa hospitali hiyo, Petro Shaluo alisema kwa miaka zaidi ya 10 aliyoitumikia hospitali hiyo alilinda mali kwa uaminifu, lakini leo anashangaa kuonekana hafai.

“Nimeitetea KCMC, niling’atwa vidole vyangu kwa ajili ya kumkamata daktari feki aliyekuwa akila fedha za wagonjwa, leo hii naonekana si kitu,” alisema mlinzi huyo.

Mkurugenzi wa rasilimali watu wa hospitali hiyo, Steven Kolimba alisema KCMC haina uwezo wa kuwalipa wafanyakazi hao, badala yake wanategemea Serikali itoe mwongozo.

Mwanasheria wa hospitali, Rachel Mboya alisema Serikali ndiyo inayohusika na malipo ya watumishi hao kwa kuwa ilikuwa inawalipa mishahara na ndiyo iliyowasitishia ajira.

Msuluhishi na mwamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Migire aliagiza kuwa ifikapo Desemba 12, mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo afike akiwa na jumla ya madai ya wafanyakazi hao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad