Wafichua Mbinu Mpya ya Ukeketaji Wasichana Wakiwa Watoto Wachanga

Wanawake wa jamii ya Watatoga  mkoani hapa wamemueleza  mbunge wa Hanang, Mary Nagu mbinu mpya ya ukeketaji inayofanywa na jamii hiyo.

Walisema kwa sasa hawawakeketi wasichana wakishabalehe bali wakiwa watoto wachanga.

Siri hiyo ilitolewa na wanawake hao wa vikundi vya ujasiriamali wanaojishughulisha na ufugaji nyuki na utunzaji wa ng’ombe wa maziwa, vinavyofadhiliwa na Shirika la Oxfam na kuratibiwa na Shirika la Ujamaa la U-CRT.

Akizungumza walipotembelewa na mbunge wao, mmoja wa wanawake hao Pascalina Michael alisema mbali na vita inayopigwa na Serikali juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini vinaendelea.

“Vita dhidi ya ukatili wa kijinsia na unyanyapaa imekuwa mkombozi kwetu wanawake lakini tunaiomba Serikali ielekeze nguvu hii katika kuwakagua watoto wanapokwenda kutibiwa au kliniki. Vitendo vya ukeketaji vinafanywa na sasa ni kwa watoto wachanga si kwa wakubwa tena,” alisema.

Alisema utekelezaji wa mradi huo wa ufugaji nyuki katika kikundi chao umekuwa na changamoto katika kuwaletea mafanikio kutokana na uhaba wa maji.

Michael alichukua nafasi hiyo,  kuiomba Serikali iwawezeshe wachimbe bwawa kwa ajili ya kupata maji ya uhakika.

Katibu Tawala Wilaya, Sarah Erasto alisema vita vya ukatili wa kijinsia kwa mwanamke vinaanza kwa wanawake wenyewe.

“Hakuna mwanaume anakuja kukeketa mwanamke ni ninyi wenyewe, lakini pia ndoa za utotoni na vipigo tuanze kukataa sisi kwanza kwa kujiunga katika vikundi kama hivi vya kuinuana kiuchumi. Unyanyapaa unaanzia pale mwanamke anapokuwa hana mchango katika jamii, lakini kumiliki uchumi unasaidia sana,” alisema Erasto.

Mbunge Hanang, Nagu alisema amefurahishwa na vikundi vya wanawake hao waliofadhiliwa na Oxfam kwa lengo la kuwakomboa katika mateso ya ukatili na unyanyapaa.

“Hilo la ukeketaji nitatafuta muda wa kuzungumza na wanawake peke yao, ila kwa sasa wanawake wenzangu chukueni silaha za vita dhidi ya ukatili na silaha hizo ni miradi ya kuwainua kiuchumi,” alisema Nagu.

By Bertha Ismail, Mwananchi bismail@mwananchi.co.tz
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad