Wanawake waliovishana pete waachiwa kwa dhamana
0
December 15, 2017
Mwanza. Washtakiwa wanne katika shauri la kufanya vitendo vinavyoashiria mapenzi ya jinsia moja na makosa la kimtandao wameachiwa kwa dhamana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza kutupilia mbali hoja za kuzuia dhamana zao zilizowasilishwa na upande wa Jamhuri.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Wilbert Chuma leo Desemba 15, baada ya kukubaliana na hoja za mawakili wa utetezi, Mashaka Tuguta, Ogastini Kulwa na Jebra Kambole kuwa hoja zilizowasilishwa na upande wa mashtaka ni dhaifu mbele ya macho ya sheria.
Washtakiwa katika shauri hilo namba 548/2017 ni Milembe Suleiman na Janeth Shonza wanaodaiwa kuvishana pete ya uchumba licha ya wote kuwa wanawake.
Wengine ni Aneth Mkuki anadaiwa kufanikisha sherehe wawili hao kuvishana pete na Richard Fabian anayeshtakiwa kwa kosa la mtandao kwa kusambaza video za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii.
Katika uamuzi wake, Hakimu Chuma amesema Mahakama haiwezi kufanyia kazi maelezo na vitu vya mashaka na uvumi kuwa washtakiwa wanaweza kudhuriwa na jamii iliyochukizwa na kitendo wanachoshtakiwa nacho.
“Ni uamuzi wa Mahakama kuwa dhamana ni haki ya washtakiwa na upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha hoja za msingi kwa nini wanyimwe dhamana zaidi ya kutoa hoja za hisia kuwa wakiachiwa watadhuriwa na jamii bila kueleza watadhurikaje na nani haswa atawadhuru,” amesema Hakimu Chuma katika uamuzi wake
Washtakiwa wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja mwenye kitambulisho na barua ya utambulisho kutoka mamlaka inayotambulika kisheria pamoja na kusaini hati ya dhamana ya Sh6 milioni. Shauri limeahirishwa hadi Januari 8, mwakani.