Wadau wa habari kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC ), wametoa tamko na kulaani kupotea kwa mwandishi wa kujitegemea wa Mwananchi, Azory Gwanda.
Tamko hilo limetolewa baada ya wadau hao wa habari likiwamo Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na THRDC kuunda kamati ndogo ya uchunguzi.
Gwanda alipotea tangu Novemba 21 mwaka huu katika mji wa Kibiti, mkoani Pwani alikokuwa akiishi na kufanyia kazi.
Akitoa tamko hilo leo Jumamosi, Katibu Mkuu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga amesema tukio hilo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na uhuru wa habari.
Aliwaomba viongozi wa siasa na Bunge kuona haja ya kulijadili suala la utekaji na kupotea kwa Watanzania ili kuja na maazimio.
"Tunaviomba vyombo vya habari viendelee kuuhabarisha uma juu ya kupotea kwa ndugu yetu Azory Gwanda,” amesema.
Kajubi ameipongeza kampuni ya Mwananchi Communications Ltd kwa kuweza kufuatilia kupotea kwa mwandishi huyo na kuvitaka vyombo vingine vya habari kuwa na moyo huo bila kujali aina ya mikataba ya waandishi wao.
Kwa upande wake mratibu wa Taifa wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa alisema wanasikitishwa na ongezeko la watu kutoweka na kwenda pasipojulikana na hakuna chochote kinachofanyika kuzuia suala hilo linalozidi kuota mizizi kwenye jamii.
"Makundi ya watetezi, waandishi, wanasiasa na wasanii wamesharipotiwa kupotea na kutoweka, kati yao wapo waliookotwa wameumizwa vibaya, wapo ambao hadi leo hawajulikani walipo na wengine kurudi wakiwa na hofu kubwa," amesema.
Ole Ngurumwa amesema wanaliomba jeshi la polisi kutoa ulinzi ili kuweza kuandamana kwa amani hadi ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP ) kupeleka hoja na kilio hicho.
Aliongeza kuwa ni lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kuhakikisha Azory anapatikana.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai aliwashukuru wadau wa habari, vyombo vya habari na watetezi wa haki za binadamu kwa kusaidia jitihada za kumtafuta Azory.
Nanai amesema inasikitisha kuona kwamba wakati Tanzania ikisherehekea miaka 56 ya Uhuru bado hakuna uhuru wa habari.
Amesema hadi sasa hakuna fununu yoyote waliyoipata juu ya tukio hilo la kutoweka kwa Azory na kuomba nguvu zaidi katika kumtafuta.