Watu 22 Wahofiwa Kufa Maji Ziwa Tanganyika

Watu 22 Wahofiwa Kufa Maji Ziwa Tanganyika
Ikiwa ni saa 40 tangu ajali ya basi na Hiace kugongana na kuua watu saba, ajali nyingine imetokea katika Ziwa Tanganyika na watu 22 wanahofiwa kufa.

Katika ajali hiyo ziwani, watu wengine 115 wameokolewa wakiwa hai baada ya boti kugonga mtumbwi jana alfajiri.

Imeelezwa kuwa miili ya watu wanne imeopolewa na imetambuliwa na ndugu zao.

Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) Mkoa wa Kigoma, Amaniel Sekulu alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea katika kitongoji cha Lubengela kijijini Msihezi, Kata ya Sunuka wilayani Uvinza.

Alisema mtumbwi uitwao Mv Pasaka uligongwa ubavuni na boti ya Atakalo Mola na kupasuka, hivyo kuzama ziwani.

Sekulu alisema mtumbwi huo ulikuwa umebeba abiria 137 waliokuwa wanakwenda kwenye mkutano wa injili katika Kijiji cha Sunuka na boti iliyokuwa ikitokea Kigoma kwenda Kalya ikiwa na abiria 65.

Sekulu alisema boti na mitumbwi inayobeba abiria hairuhusiwi kufanya safari usiku.

Akizungumzia ajali hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Sweetbert Njewike alisema wanaendelea kuwatafuta watu ambao hawajaonekana waliokuwa wakisafiri na vyombo hivyo.

Alisema shughuli za uokoaji zinafanywa kwa pamoja na vikosi vya Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba kulikuwa na dosari zilizosababisha ajali hiyo.

Alizitaja dosari hizo kuwa ni ukosefu wa vifaa vya uokoaji, vya kuzima moto na boti kufanya safari usiku.

Diwani wa Sunuka, Athumani Chuma alisema ajali hiyo imeacha simanzi kutokana na mazingira iliyotokea.

Alisema licha ya ajali kutokea saa tisa usiku, wanakijiji walionyesha mshikamano katika kuokoa watu wakiwa hai na hatimaye kuopoa maiti nne.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msihezi, George Gasper alisema ajali ilitokea umbali wa mita takriban 150 kutoka ufukweni, ikiwa ni muda mfupi baada ya boti la Atakalo Mola kushusha na kupakia abiria katika Kitongoji cha Lubengela.

Desemba 20, watu saba walikufa papohapo na wengine 12 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Saratoga kugongana uso kwa uso na gari ndogo la abiria.

Ajali hiyo ilitokea saa 4:30 asubuhi katika Kijiji cha Kabeba katani Mwakizega wilaya hiyohiyo ya Uvinza.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad