Tafiti inaonyesha kuwa watu wazima na watoto wa rika zote wapatao milioni 1.4 wanaishi na virusi vya Ukimwi nchini Tanzania ambao ni sawa na asilimia 2.9 ya watu wote bila kujali umri wao.
Matokeo hayo yanatokana na utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi Tanzania (THIS) ya mwaka 2016/2017 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambao unaonyesha kiwango cha virusi vya Ukimwi nchini kwa watu wazima wenye umri wa miaka 15-49 hii ni asilimia 4.7 wanaishi na VVU.
Utafiti huo uliofanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na kuhusisha Kaya 14,811 zinaonyesha kuwa vijana walio kwenye umri huo (15-24) wengi wao wakiwa wasichana wanapata maambukizi mapya.
Takwimu hizo zimeonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15-19 ni asilimia 0.7 ambapo asilimia 1.0 ni watoto wa kike na asilimia 0.4 ni watoto wa kiume.
Kwa vijana wenye umri wa miaka 20-24 kiwango hicho kimeongezeka na kuwa asilimia 2.2 wasichana wakiwa ni asilimia 3.4 na wanaume ni asilimia 0.9.
Kwa upande wake Mama Samia alisema, “naomba wasichana wabadilike Ukimwi ukikutesa hautakutesa peke yako bali Taifa zima, takwimu hizi zinaonyesha hali si nzuri kwa kundi hili ambalo ndio nguvu kazi ya Taifa, mjitahidi muwe na mienendo inayoeleweka.”