Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Bw. Julius Mseleche Kaondo, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za rushwa.
Akiongea na wanahabari ofisini kwake mjini Dodoma, Mh. Jafo amesema kuwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi huyo kutokana na mamlaka aliyopewa chini ya kifungu Na. 4 (1-5) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka na Wilaya) sura 287 kwa mujibu wa Kanuni ya 36 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.
Mkurugenzi huyo anatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa katika mchakato wa zabuni ya miradi ya Maji na kushindwa kusimamia manunuzi katika utekelezaji wa miradi ya maji, katika kijiji cha Kamwanda Wilayani Nkasi, Mkoani Rukwa na kusababisha mradi huo kutokamilika kwa wakati.
Mhe. Jafo amesema mradi huo ulikuwa ukigharimu shilingi bilioni 7 na wenye lengo la kutatua kero ya Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na kuwaletea maendeleeo wananchi wa wilaya hiyo.
Aidha Waziri Jafo ametoa wito kwa Wakurugenzi , Wakuu wa Idara, pamoja na watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.kwa kushindwa kusimamia hatua za manunuzi.