Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), na Watendaji wa Mamlaka mbalimbali nchini wametakiwa kusimamia sheria ili kuhakikisha kuwa wanadhibiti changamoto za uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua barabara ya Dodoma-Mayamaya-Mela-Bonga (Babati), KM 231.5 ambapo amesema kuwa mamlaka zote hizo zikishirikiana kwa pamoja katika suala zima la ulinzi na utekelezaji wa sheria kutasaidia miundombinu hiyo kudumu kwa muda mrefu.
“Vitendo kama vya umwagaji wa mafuta ya magari kwenye barabara, kupiga jeki, kuswaga wanyama, kuchimba kokoto na mchanga kwenye madaraja vinachangia sana uharibifu wa barabara, hivyo simamieni kuhakikisha vitendo hivi vinakoma mara moja”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa,amewataka madereva kufuata alama za kudhibiti mwendo (spidi) zilizoko barabarani hususani katika kipindi hiki cha sikukuu kwani kutokufuata sheria hiyo kunapelekea ajali nyingi za barabarani.
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa ameipongeza TANROADS na Kampuni ya Mkandarasi ya CHICO kwa kuhakikisha kuwa barabara hiyo na daraja kubwa la Kelema lenye urefu wa mita 205 lililopo kwenye barabara hiyo linakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, amesema kuwa barabara hiyo imekamilika kwa asilimia 98 ambapo kazi zinazofanyika sasa ni uwekaji wa kingo na alama za barabarani hivyo amefafanua kuwa kazi hiyo inatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Barabara ya Dodoma-Mayamaya-Mela-Bonga (Babati), yenye urefu wa kilometa 231.5 ambayo imejengwa kwa takribani shilingi Bilioni 257.6 inatarajiwa kufunguliwa mwakani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.