mMwanamke mkazi wa Kijiji cha Mayenzi wilayani Ngara anatuhumiwa kumuua mke mwenza na kumzika shambani.
Kifo hicho kinachodaiwa ni kutokana na wivu wa mapenzi kimetokea katika Kata ya Kibimba mkoani Kagera ambako aliyeuawa alizikwa kwenye shamba la viazi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mayenzi, Philipo Rutumbanya amesema Edina Joseph (28) anatuhumiwa kumuua Noelina Joseph (24).
Wawili hao ni wake wa Joseph Laurean (33), mkazi wa Kijiji cha Mayenzi wilayani Ngara.
Rutumbanya amesema mauaji hayo yalifanyika jana Jumatano Desemba 13,2017 saa 7:30 mchana na kwamba mtuhumiwa amefikishwa polisi.
Amesema Edina alihisiwa kuhusika na mauaji baada ya mumewe kumkuta akiwa na damu mwilini shambani.
Mwenyekiti huyo wa kijiji amesema Laurean alipomhoji mkewe hakujibu lolote na alipofuatilia shambani aliona nguo za mkewe mdogo lakini yeye hakuwepo.
Amesema Laurian alitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ndipo mtuhumiwa Edina alipohojiwa na alieleza alikuwa na chuki na mke mwenzake aliyeolewa miezi miwili iliyopita.
Mwenyekiti huyo amesema walimweka Edina chini ya ulinzi na aliwapeleka kwenye shamba la mume wake ambalo ni mali ya binamu yake John Shimimana alikoonyesha alikomzika mwenzake kwenye tuta la viazi.
Akizungumzia tukio hilo, mume wa wake hao, Laurian amesema ameishi na Edina kwa miaka 12 na wamejaliwa watoto watano; wa kike mmoja na wa kiume wanne. Pia ni mjamzito.
Laurian amesema mkewe mdogo alimpangia nyumba katika Kijiji cha Kanazi umbali wa kilomita sita kutoka Kijiji cha Mayenzi na alimpatia shamba ambalo alipewa na binamu yake Shimimana, ambaye ni diwani wa Kata ya Kibimba.
Amesema alipotoka matembezi kijijini alifika nyumbani kwa Edina alikokuwa amelala Jumanne Desemba 12,2017 lakini hakumkuta.
Laurian amesema alikwenda kumuona mkewe mdogo Noelina aliyekuwa shambani ambako alimkuta Edina akiwa na jembe na mwili ukiwa na damu.
Amesema alipomhoji kuhusu damu alitetemeka na alipofuatilia alikuta nguo za Noelina lakini yeye hakuonekana.
"Tangu nioe mke wa pili kumekuwa na malumbano na malalamiko lakini niliona kawaida sikutarajia kama angechukua uamuzi wa kumuua mwenzake," amesema Laurian.
Polisi wilayani Ngara imefika eneo la tukio ambako Edina amekamatwa na baada ya kupata kibali cha Mahakama ya Wilaya ya Ngara mwili wa Noelina umefukuliwa.
Akizungumza wakati wa kufukua mwili ofisa upelelezi wa Polisi wilayani Ngara, Edward Masunga amewataka wananchi wakiwemo wanandoa kufuata utaratibu wa kufikisha malalamiko kwa viongozi wa vijiji badala ya kujichukulia sheria mkononi.