Hoja ya kuongezwa muda kwa Rais wa Tanzania imeibukia katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambako mwakilishi ameshauri Rais wa Zanzibar aongezewe miaka miwili ili atawale kwa miaka saba.
Awali, hoja kama hiyo iliibuliwa na mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia aliyesema ni vyema yakawepo marekebisho ya Katiba ili kuruhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atawale kwa miaka saba, hoja ambayo bado hajaipeleka bungeni.
Hata hivyo, tofauti na Nkamia ambaye bado hajawasilisha hoja yake, mwakilishi wa Shaurimoyo, Hamza Hassan Juma yeye ameifikisha barazani akishauri Serikali ya Zanzibar kuwasilisha marekebisho ya Katiba ili Rais wa Zanzibar atawale kwa miaka saba.
Hamza alitoa ushauri huo jana katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akichangia muswada wa sheria ya marekebisho ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 1984.
Alisema kuwa ili kumpa Rais wakati mzuri wa kuwatumikia wananchi ipasavyo, hakuna budi muda wake ukaongezwa kwa miaka miwili zaidi.
Mwakilishi huyo alisema muda wa miaka mitano wa uongozi wa Rais madarakani ni mdogo na Taifa hupoteza fedha nyingi za wananchi kwa kufanya uchaguzi kila miaka mitano, hivyo ni vyema Serikali ikalifanyia kazi suala hilo. Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa tathmini yake ya Uchaguzi Mkuu, fedha za walipakodi zinazotumika zinaweza kujenga zaidi ya shule kubwa 20 ambazo zingesaidia jamii kuondokana na upungufu uliopo.
Hamza alisema pamoja na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar kuweka muda wa miaka mitano, lakini kuna nafasi ya kuongeza muda kwa Rais wa Zanzibar pindi baraza hilo likiridhia kufanya hivyo kwa masilahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla. “Kwa kuwa Katiba ya Zanzibar inajitegemea, hivyo ni wazi kuwa tunaweza kufanya hivyo pasi ya kuathiri lolote katika Katiba ya Tanzania juu ya kuongeza muda wa kiongozi huyo,” alisema mwakilishi.
Akichangia muswada huo, mwakilishi wa Welezi, Hassa Khamis Hafidh alitaka kuongezewa nguvu Tume ya Uchaguzi ili kuepusha baadhi ya watu kujitangaza kabla haijatoa matokeo rasmi.
Akiwasilisha muswada huo, waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed alisema lengo ni kuifanya sheria hiyo kwenda na wakati uliopo.