Aingia Matatizoni Baada ya Kuokota Sarafu ya Majini Akijua Dhahabu

Aingia Matatizoni Baada ya Kuokota Sarafu ya Majini Akijua Dhahabu
UKISTAAJABU ya Musa, utaona ya Firauni! Mwanaume mmoja mkazi wa Chamazi, Dar, Jafari Daudi amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuokota pesa ya majini (sarafu) ambayo inamtesa na kutamani kuikimbia nchi, Risasi Mchanganyiko linakupa habari kamili.

Akisimulia kwa huzuni, mwanaume huyo mwenye mke na mtoto mmoja alisema kuwa, miaka mitatu iliyopita alikuwa akifanya kazi maeneo ya Kijiji cha Mbondole, Kata ya Msongola, Dar ambako ndiko mkasa huo ulikompata.

Alisema kuwa, siku moja akiwa anaelekea kazini, aliokota sarafu ambayo ilikuwa iking’aa kama dhahabu ambapo alipoiangalia vizuri aliiona kama zile pesa za zamani, akaiweka mfukoni mwa suruali na kuelekea kazini kwake.

Jafari alisimulia kuwa, aliendelea na kazi, lakini ghafla alianza kuumwa na kichwa kupindukia huku jasho likimtoka na wakati huohuo baridi ya ajabu hivyo kutia shaka kuwa huenda hali hiyo ilimpata kutokana na pesa aliyoikota hivyo aliamua kufunga ofisi na kurudi nyumbani.

“Nilifika nyumbani na kumweleza mke wangu nilivyoiokota hiyo pesa, nikamuonesha, sikushughulika nayo tena, nikaendelea na mambo mengine maana baada ya kufika nyumbani tu nilipona kabisa.

“Niliendelea na maisha, lakini ghafla nilifukuzwa kazi na kila nilipokuwa ninakwenda kuomba kazi sipati hadi sasa huku kichwa kikinisumbua sana na kila siku usiku ninaota ndoto za ajabu ambapo ninachukuliwa na dada mrembo ambaye ananipeleka baharini ambako anasema ndiyo kwao.

“Mke wangu alinishauri niirudishe hiyo pesa nilikoiokota ambako niliipeleka palepale na kuiacha, lakini cha ajabu nilipofika nyumbani, wakati mke wangu ananiandalia chakula, akaikuta ipo katikati ya kitanda.

“Niliichukua tena na kwenda kuitupa, lakini iling’ang’ania kwenye mkono, nikashindwa kuitupa na kurudi nayo nyumbani.

“Siku moja mwanangu aliichukua na kwenda nayo dukani ambako alirudi na juisi na chenji 9,500 ndani yake hiyo pesa ikiwepo, usiku wake nikaoteshwa kwamba hiyo pesa akichukua mtoto wa chini ya miaka mitatu na kwenda nayo dukani, itaonekana ni elfu kumi na atarudishiwa yenyewe pamoja na chenji,” alisema Jafari.

Aliendelea kuelezea kwamba amekuwa akipambana na mauzauza mengi ikiwa ni pamoja na kuumwa kichwa huku pia akishindwa kumtimizia haki ya unyumba kikamilifu mkewe ambaye naye anataka kumkimbia.

“Ndoa yangu iko kwenye hatari kubwa ya kuvunjika kwani kila kukicha mke wangu ananiambia ataondoka, sasa ninashindwa hata nifanyeje maana ni majanga makubwa haya, nimeshaenda kwa waganga wengi, lakini wameshindwa kunisaidia,” alisema Jafari.

INA THAMANI YA MAMILIONI

Jafari alisema kuwa, amewahi kumwonesha hiyo pesa Mzungu mmoja ambaye alikwenda na vifaa vya kupima na kusema ina thamani ya shilingi milioni 270 za Kitanzania hivyo akaahidi kwenda kuichukua na kumpa hizo fedha, lakini hajawahi kumuona tena.

AWAANGUKIA WATANZANIA

“Jamani Watanzania wenzangu, kama kuna mtu anaweza kunisaidia ili niondokane na tatizo hili, ninamuomba aje anisaidie maana ninateseka. Sina raha wala amani maishani mwangu, sijielewi kama mimi ni binadamu kama wengine au siyo.”
Chanzo: Global Publisher
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad