Mwanaume mmoja mwenye miaka 40 katika kijiji cha Kirimon anashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini Kenya baada ya kujaribu kumuoza mwanaye wa miaka 4 kwa mzee wa miaka 70 jana January 2, 2017 baada ya mpango wake kushtukiwa na Tume ya Taifa ya Huduma za Watoto nchini humo.
Inaelezwa kuwa mpango huo ulivurugika baada ya mama wa mtoto na majirani kutoa taarifa kwa tume hiyo. Kwa mujibu wa Afisa wa tume hiyo Jane Kabiro, mwanaume huyo alitaka kupata ng’ombe 40 kwa kumuoza mwanaye huyo ili afidie ng’ombe aliowatoa kama mahari pindi alipomuoa mkewe ambaye ni mama wa mtoto huyo.
Kabiro alieleza pia kuwa siku za nyuma kidogo mwanaume huyo alitaka kuoa mke wa pili na mkewe alipokataa suala hilo alimfukuza na watoto warudi kwa mama mkwe wake. Baada ya mwanamke huyo na wanaye kwenda kuishi kwa mama yake alikwenda kuleta vurugu akitaka kumuoza mwanaye kama fidia ya mahari aliyotoa alipomuoa mwanamke huyo.