ARSENAL chini ya kocha wake Arsene Wenger inapambana kuhakikisha inamsajili straika Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani.
Aubameyang raia wa Gabon anatakiwa na Arsenal kwa udi na uvumba ili kuziba nafasi ya straika Alexis Sanchez ambaye anatarajiwa kujiunga na Manchester United au Manchester City.
Maisha ya Aubameyang katika Klabu ya Borussia Dortmund sasa siyo mazuri na inaonekana wazi straika huyo anataka kuondoka na klabu iliyoonyesha nia ya kumsajili ni Arsenal.
Wenger hana jinsi zaidi ya kumuachia Sanchez kwenda jijini Manchester kwani isipofanya hivyo sasa, inaweza kumtoa bure katika usajili ujao kabla ya msimu mpya.
Hata hivyo zipo sababu zinazoonyesha kuwa, Aubameyang anaweza kuisumbua Arsenal kutokana na sababu zifuatazo:
#5 Kulazimisha ushindi
Aubameyang anajua kufunga na akiwa karibu na lango ni mtu hatari sana kwa wapinzani. Hata hivyo, ana tatizo la kutokuwa mpambanaji kwa ajili ya timu na hana njia nyingi za kuwabuguzi mabeki, akishindwa njia moja ndiyo basi tena. Anategemea kufunga kwa kutengenezewa nafasi na wakishindwa kumfanyia hivyo ndiyo basi tena.
#4 Tatizo la ulinzi
Moja kati ya matatizo makubwa ya Aubameyang awapo uwanjani ni mchango wake wa kukaba. Kwa soka la sasa hasa England, kukaba ni kazi ya mshambuliaji pia ili kupunguza kasi ya adui. Sasa Aubameyang yeye si mzuri katika kukaba hivyo atapata tabu katika mfumo huo.
#3 Hayupo kama zamani
Aubameyang wa sasa si yule wa msimu mmoja au miwili nyuma, ameshuka pia vituko vyake nje ya uwanja ni tatizo kichwani mwake. Sawa, sasa anaweza kuwa amefunga mabao 21 katika mechi 23 msimu huu, lakini hailingani na nafasi anazopoteza uwanjani sasa katika kikosi cha Borussia Dortmund.
#2 Gharama yake haiendani na umri
Aubameyang sasa ana umri wa miaka 28, hivyo dau la Borussia Dortmund la kumuuza kwa pauni milioni 53 (Sh bilioni 162.8), haiwezi kuwa na faida kwao kwani hatoweza kucheza kwa ushindani kwa muda mrefu. Hii ina maana kuwa, Arsenal haitaweza kumtumia kwa muda mrefu.
#1 Hawezi kuwa Alexis Sanchez
Ukweli ni kwamba, Aubameyang hawezi kuwa mbadala sahihi wa Alexis Sanchez. Arsenal inadhani Aubameyang ndiye mbadala sahihi wa Sanchez lakini ukweli ni kwamba wawili hao wapo tofauti kabisa. Aubameyang anacheza kwa mtindo mmoja na kwa kutumia upande mmoja tu lakini Sanchez yupo pande zote. Hapa ndipo Arsenal inapoongeza nguvu pia kumnasa Malcom wa Bordeaux.