Azamu Yawaahidi Ushindi Mashabiki Wake

Nahodha wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, amewahakikishia mashabiki wa timu hiyo kuwa wataendelea kulinda heshima ya Uwanja wa Azam Complex kwa kuhakikisha wanaifunga Yanga SC na kuzoa pointi zote tatu.



Azam FC itakuwa kwenye vita kali ya kuwania kilele cha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) leo siku ya Jumamosi majira ya saa 10.00 jioni pale watakapowakaribisha Wanajangwani hao, ambapo ushindi wowote utaifanya kufikisha jumla ya pointi 33  na kuongoza ligi kwa pointi moja dhidi ya Simba, ambao watakuwa na mchezo mmoja mkononi.

Akizungumza hapo jana na wandishi wa habari kuelekea mchezo huo, Mao amesema anaamini ya kuwa yeye pamoja na wachezaji wenzake watakaopata nafasi ya kucheza basi wataiwakilisha vema timu hiyo na kupata matokeo.

“Sisi kama Azam FC daima tunapocheza mechi za hapa nyumbani huwa hatuna presha japo tunajua nini tunatakiwa tukifanye, kwa hiyo mechi ya nyumbani mtu anakuja nyumbani kwetu tunamkaribisha lakini anatakiwa ajue haitakuwa rahisi,” amesema Mao.

Huo ni mchezo wa kwanza kihistoria kwa Azam FC na Yanga kupigwa katika uwanja huo, baada ya msimu huu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuridhia mechi zote zinazoihusu timu hiyo watakapokuwa nyumbani dhidi ya Simba na Yanga zipigwe ndani ya viunga hivyo vya Azam Complex, badala ya utaratibu wa awali zote zikipangwa kufanyika Uwanja wa Taifa au Uhuru.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, naye hakuwa mbali kukielezea kiufundi kikosi chake, akidai vijana wake wako kwenye hali nzuri na anachoamini ni ushindi katika mchezo huku akikiri kuiheshimu Yanga kutokana na ukongwe wao.

“Vijana wako vizuri na wako katika maandalizi mazuri na kiafya, kiakili wako vizuri na wanataka kuwahakikishia mashabiki wao kesho kuwa wanatimiza ile adhma yao katika kulinda heshima ya uwanja wetu wa Azam Complex kwamba hatuhitaji kufungwa hapa na kesho vijana wako sawa na watafanya lile tulilolipanga nao,” alisema.

Azam FC itaingia kwenye mtanange huo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka kuifunga Tanzania Prisons mabao 2-0 katika mchezo wake wa mwisho wa ligi uliofanyika Uwanja wa Sokoine, mjini Mbeya, huku Yanga yenyewe ikiifunga Ruvu Shooting bao 1-0.

Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kombe la Mapinduzi mwaka jana na mwaka huu, watanufaika na urejeo wa mshambuliaji wake anayetoka kwenye majeruhi Mbaraka Yusuph huku beki Daniel Amoah, akiwa kwenye hatua za mwisho za kuanza kuonekana tena dimbani baada ya kupona majeraha yake ya goti.

Kihistoria timu hizo zimekutana mara 18 kwenye mechi za ligi, Azam FC ikiwa imeshinda mara tano na Yanga ikiibuka kidedea mara sita huku ikishuhudiwa mechi saba wakitoka sare, ambapo katika mchezo wa mwisho Yanga ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Obrey Chirwa.

Hadi sasa Azam FC ikiwa inahitimisha raundi ya kwanza ya ligi leo kwa mechi ya 15, imefanikiwa kushinda mechi nane na kutoka sare mara sita huku ikiwa haijapoteza mechi hata moja na ikiwa ndio timu pekee iliyofungwa mabao machache baada ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne na ikifunga 15.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad