Baada ya Babu Seya na Mwanaye Kwenda Ikulu Mjadala Mkali Waibuka
0
January 04, 2018
Inawezekana ilikuwa ni nia njema kwenda kumshuku Rais kwa kumpa msamaha uliomuepusha na kifungo cha maisha, lakini kitendo hicho cha Nguza Mbangu Viking na wanawe kimepokelewa kwa hisia tofauti.
Nguza, ambaye ni mtunzi wa wimbo maarufu wa “Seya” uliomfanya apachikwe jina la Babu Seya katika kesi ya kubaka na kulawiti wanafunzi wenye umri kati ya miaka sita na nane, na mwanae Johnson Nguza au Papii Kocha, walisamehewa na Rais John Magufuli pamoja na wafungwa wengine 8,150 siku ya Uhuru wa Tanganyika.
Alikuwa kitumikia kifungo cha maisha baada ya mahakama kumtia hatiani kwa kubaka na kulawiti watoto hao, na juhudi za kupangua hukumu hiyo Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na nyuingine za nje hazikuweza kufanikiwa.
Lakini msamaha wa nadra kutokea kwa wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha na wenye makosa ya kubaka na kulawiti, ulimuepusha nyota huyo maarufu kwa kupiga gitaa la solo na mara tu alipotoka alisema angependa kuonana na Rais kwa ajili ya kumshukuru na akapata nafasi hiyo juzi.
Lakini kupokelewa kwake kumeibua hoja tofauti.
Wako wanaowaangalia waliofanyiwa vitendo hivyo miaka 13 iliyopita, ambao kwa sasa ni wasichana, na wengine wanaoangalia nafasi waliyoipata tofauti na wengine walionufaika na msamaha huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watu waliohojiwa na gazeti hili walisema tukio la kwenda Ikulu halikupaswa kupambwa, pamoja na ukweli kwamba Katiba inampa Rais mamlaka ya kusamehe wafungwa wa aina yoyote.
“Sikuona haja ya Ikulu kulikuza suala la wanamuzi hao kwenda kuonana na Rais. Baada ya kusamehewa kwa nini wanageuzwa kama mashujaa?,” alihoji Wakili Onesmo Kyaule.
“Inawezekana kabisa hilo likawa na picha tofauti kwa watu waliofanya au watakaofanya makosa kama yao.”
Ikulu ilisambaza picha za Nguza na familia yake wakiwa wanatembea kuelekea Ikulu na baadaye wakiwa kwenye mazungumzo na Rais na nyingine zinazoonyesha wakisalimiana na baadaye wakitoka.
Dk Kyauke alisema licha ya sheria kumpa Rais mamlaka ya kusamehe, wanamuziki hao walipaswa kurejeshwa kwao baada ya kusamehewa.
Naye wakili mwingine wa kujitegemea, Alloyce Komba wa kampuni ya Haki Kwanza, alipinga kitendo cha wanamuziki hao kwenda Ikulu kwa maelezo kuwa licha ya kusamehewa kwao, bado wana hatia ya ubakaji.
Alisema lingekuwa jambo la maana kama wangeitisha mkutano na waandishi wa habari na kumshukuru Rais kuliko kwenda Ikulu na suala lao kutangazwa.
“Rais akisamehe wafungwa anakuwa na vigezo vyake ila katika hili la kina Babu Seya, nimeshtuka kidogo,” alisema.
Alibainisha kuwa Papii Kocha na Babu Seya walitiwa hatiani na hata walipokata rufaa walishindwa.
“Kwa kuwa tunaheshimu utawala wa sheria na Mahakama ndio yenye uamuzi wa mwisho na wahusika wameshindwa kwenye hizo ngazi zote, tunatakiwa tuheshimu,” alisema.
“Kwenda Ikulu kuna heshima, hawa heshima hii wameipata wapi? Aaah sisi tunaomuamini Mungu tunasema sawa ila katika sheria, sheria ni sheria.”
Alisema msamaha huo unaweza ukawa kikwazo kwa vyombo vya Serikali vinavyopambana kudhibiti makosa ya ubakaji na mengineyo.
Naye Profesa Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) alisema: “Sikutegemea kama wangeenda Ikulu kwa sababu msamaha wa Rais haufuti hukumu. Hauondoi jinai waliyofanya.
“Sijasikia kama wameomba radhi nasema hivi kwa sababu watoto waliotendewa vitendo hivyo pamoja na wazazi wao bado wapo na wanaliona suala hili.”
Alisema kama wanamuziki hao wangekaribishwa Ikulu sambamba na waliotendewa vitendo viovu walau ingeeleweka, “hata Serikali kufikiria fidia kwa waliotendewa vitendo vile nayo ingeweza kueleweka”.
Kwa upande wake, Dk James Jesse wa Shule Kuu ya Sheria Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) pia alisema msamaha haujafuta kosa.
“Unapopewa msahama sio kwamba kosa lako linafutwa. Rais ana mamlaka ya Kikatiba kufanya alichokifanya na kama watu watawaza tofauti huwezi kuwazuia,” alisema.
Tags