Klabu ya Kagera Sugar kupitia kwa Mratibu wake, Mohamed Husein amesema kuwa timu hiyo kamwe haita muadhibu beki wake kisiki, Juma Said Nyoso kufuatia tukio lake la kumpiga shabiki mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba uliyofanyika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoka siku ya Jumatatu ya Januari 22, mwaka 2018.
Mratibu huyo, Husein ameyasema hayo kupitia mtandao wa michezo wa Shaffi dauda, Kagera Sugar haitochukua hatua zozote zile za kinidhamu dhidi ya beki wao Juma Nyoso ambaye ametoka Polisi kwa dhamana na tayari anaendelea na mazoezi.
“Jambo hili sisi tunaliangalia kwa macho mawili, kwanza tuweke wazi msimamo wetu, sisi hatutompa adhabu yoyote Nyoso kwa sababu yule shabiki alimkosea mchezaji wetu pamoja na Nyoso kuonekana kuwa na tabia ya ukorofi lakini kwa hili yule shabiki alimkosea na mimi nilishuhudia.”
“Kumpulizia mtu vuvuzela kwenye sikio haikuwa sawa lakini wakati huo mchezaji ndio ametoka uwanjani kucheza, lakini shabiki huyo alikuwa akimshabulia Nyoso kwa matusi hata wakati mchezo unaendelea na wakati wa mapumziko bado aliendelea kumtukana sasa na yeye ni binadamu alighadhabika.”
“Shirikisho na polisi wao ndio wataona nini cha kufanya kwa hiyo sisi tunasubiri kuona polisi wataamua nini kama kwenda mahakamani au kumalizana nje ya mahakama sisi tupo tayari. Kijana ameachiwa kwa dhamana na sasa anaendelea na mazoezi na wenzie.”
Inadaiwa shabiki huyo alitoa kauli chafu na za kuudhi kwa Nyoso pamoja na kumpigia kelele za vuvuzela kabla ya Nyoso kuamua kumpiga.