KIUNGO wa Yanga, Pius Buswita atakosa mchezo dhidi ya Azam kutokana na adhabu ya kadi tatu za njano huku Kelvin Yondani akirejea baada ya adhabu yake kumalizika.
Jumamosi ijayo, Azam FC itavaana na Yanga mchezo ambao utapigwa katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja wa Yanga Hafidhi Saleh alisema Buswita na Andrew Vincent ‘Dante’ watakosekana kutokana na kupata kadi katika michezo tofauti.
“Ni kweli Buswita kwenye mchezo dhidi ya Azam hatakuwepo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano ambazo alipata kwenye michezo iliyopita pamoja na beki Andrew Vincent ‘Dante’.
“Lakini pia Yondani amemaliza adhabu yake hivyo atakuwepo uwanjani,” alisema Saleh ambaye anaheshimika miongoni mwa wanachama na viongozi wa Yanga.