Baada ya kuwapo kwa uhaba wa mafuta visiwani hapa kwa takrban wiki moja sasa, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji Zanzibar (Zura) imesema uhaba huo umechangiwa na ongezeko la matumizi ya nishati hiyo katika sherehe za sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, kaimu mkuu wa kitengo cha uhusiano wa mamlaka hiyo, Khuzaimat Bakari Kheri alisema wananchi wengi wametumia nishati hiyo katika kipindi hicho na kuvuka makadirio yaliyopagwa na mamlaka kwa mafuta yanayoingia Zanzibar.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za mamlaka hiyo, wastani wa mafuta ya petroli yanayotumika kwa siku ni lita 165,000, dizeli lita 152,000 na mafuta ya taa lita 163,000 na kwamba katika kipindi hicho cha sikukuu, utumiaji huo uliongezeka maradufu. Hata hivyo, hakutaja kiwango halisi cha ongezeko hilo akisema bado wanafanya utafiti ili kuona uhalisia pamoja na kuchukua hatua madhubuti.
Mbali ya ongezeko hilo la matumizi, Khuzaimat alisema sababu nyingine iliyochangia huduma ya mafuta kuadimika visiwani hapa ni uchakavu wa miundombinu ya bandari ya mafuta iliyopo Maruhubi, Unguja hali ambayo inachangia baadhi ya meli kubwa za mafuta kushindwa kutia nanga.
Alisema kutokana na hali hiyo, meli hizo hulazimika kufunga gati katika Bandari ya Dar es Salaam au Mombasa Kenya, kisha Zanzibar hutoa meli ndogo kwa ajili ya kuyachukua na kuyafikisha visiwani hapa hali hiyo inayosababisha usumbufu.
“Mfano mdogo, tangu tarehe 29 mwezi uliopita kuna meli kubwa ya mafuta ya Zanzibar imekuja lakini imeshindwa kushusha na kulazimika kwenda kuyashushia Mombasa, huku meli ya kampuni ya Gapco nayo ikiwa hukohuko ikisubiri mafuta hayo ili kuja nayo Zanzibar, hili ni wazi kuwa kama tungekuwa na bandari nzuri meli hiyo kubwa ingeshusha hapahapa na kuondokana na usumbufu huu,” alisema.
Khuzaimat alisema kutokana na hali hiyo, Zura ipo katika mipango imara ya kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi ikiwamo kufanya mazungumzo na wahusika wakuu wa bandari ili kuona inajengwa vizuri ili kuwezesha meli kubwa kutia nanga na kushusha mafuta bila tabu.
Baadhi ya wamiliki wa vituo vya kuuzia mafuta visiwani humu walisema pamoja na matumizi makubwa ya mafuta katika kipindi cha sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya, lakini kama kungekuwa na miundombinu imara ya bandari ni wazi kuwa shida hiyo ingeondoka bila ya wasiwasi.
Meneja wa kituo cha mafuta cha Kijangwani Zanzibar, Abubakar Mohamed alisema ni masikitiko makubwa kuona hali hiyo bado inaendelea bila kutafutiwa ufumbuzi unaofaa.
Alisema pamoja na wao kukosa mapato yatokanayo na mauzo kwa muda huo, lakini pia wamekuwa wakipokea malalamiko kwa wateja wao kutokana na hali hiyo kuwa ngumu hasa kwa upande wa wenye magari ya abiria.
Othman Ali ambaye ni dereva wa gari la abiria alisema pamoja na kuwa katika kipindi hiki kuonekana kazi kuwa nzuri, lakini uhaba wa mafuta umerudisha nyuma malengo yao.