Kuna aina mbalimbali za kuku ambazo mfugaji anaweza kufuga na kila aina inategemeana na malengo ya mtu husika anayetaka kufanya shughuli hii ya ufugaji, hivyo leo nimekuletea makundi makuu manne ya kuku ambayo tunayafuga hapa Tanzania.
KUKU WA NYAMA.
Hii ni moja ya kundi la kuku ambalo linafugwa sana hapa nchini na kuku hawa wanafugwa kwa malengo ya kuzalisha nyama tu. Uzalishaji wa kuku hawa wanachukuliwa kuku wazazi kutoka nje ya nchi na kuhifadhiwa sehemu maalumu kwa ajiri ya kuzalisha mayai na mayai yanatotoreshwa na kupata vifaranga kwa ajili ya nyama ,
Faida ya kuku hawa.
Faida ambayo utaipata kama mfugaji ni kuwa kuku hawa hufugwa kwa mda mchache muda wa miezi miwili au mitatu na kuuzwa kwa ajili ya matumizi ya nyama, hivyo ni sehemu nzuri yakujipatia kipato na kunufaika na ufugaji wako kwa muda mfupi.
Zingatia.
Gharama za kuwalea kuku hawa ni kubwa kidogo hivyo unapoamua kufanya ufugaji kwa ajili yakupata tija katika kukuza kipato chako ni muhimu ukafuga kuku wengi kwa wakati mmoja hii itakufanya upate faida nzuri kuliko kufuga kuku wachache na ukapata hasara na kuona ufugaji haulipi kumbe wewe mwenyewe haukuwa na taarifa kamili kuhusu ufugaji wako.
Muhimu.
Ni muhimu sana kutunza kumbukumbu za gharama za matumizi katika mradi wako wa kuku ili pale utakapo uza uweze kujifanyia tathmini na kujua umepata faida au hasara katika mradi wako.
KUKU WA MAYAI.
Hawa ni aina ya kuku ambao hufugwa kwa malengo maalumu ili kuzalisha mayai, kuku hawa wanataga kwa wingi sana mayai na wanataga bila jogoo, kuku hawa wamendaliwa vizuri kwa ajili ya kutaga tu hivyo kama utaamua kuwawekea jogoo watataga na kuatamia lakini vifaranga wake watakuwa hawana ubora ule unaotakiwa.
Faida ya kuku hawa.
Zingatia.
Ili kupata faida iliyokusudiwa katika mradi wako huu wa kuku unatakiwa uwape chakula bora na cha kutosha pia uzingatie chanjo na tiba kwa magonjwa pale unapoona dalili ya magojwa.
Muhimu.
Ufugaji wakuku ni moja ya aina ya miradi yenye faida nzuri iwapo tu mfugaji atazingatia kanuni bora za ufugaji. Ufugaji huu ili ukuletee tija ni muhimu ukafuga kuku wengi angalau mia tatu na kuendelea hapo utaiona faida yake nzuri.
KUKU CHOTARA.
Hawa ni aina ya kuku ambao wamechanganya aina fulani ya kuku na aina nyingine ya kuku na kupata aina moja ya kuku, mfano: amechukuliwa jogoo wa kienyeji akachanganywa na tetea wa kisasa na vifaranga vitakavyotoka vitakuwa chotara kwa maana watakuwa na sifa baadhi za kienyeji na sifa baadhi za kisasa.
Kuku hawa kwa hapa nchini wapo wengi na kuna makundi mbalimbali ya kuku kulingana na asili na mahali walipo tokea, mfano: MALAWI, KENBRO, SASO na KROILA na hawa wanatofautiana sifa na asili.
Faida ya kuku chotara.
Hapa nitataja kwa ujumla faida zote ila wakati mwingine nitachambua aina moja moja ya kuku chotara.
Wanakuwa kwa haraka na wanakuwa na maumbo makubwa tofauti na kuku wakienyeji hivyo ni wazuri sana kwa nyama.
Ni watagaji wazuri sana tofauti na kuku wakienyeji (kuku hawa ukuwahudumia vizuri wanataga mayai kati ya 180-300 kwa mwaka hivyo ni wazuri sana kwa mayai.
Wanaishi kwenye mazingira yeyote yale kwa maana wanaweza kuishi vizuri wakiachiwa kujitafutia chakula.
Wanastahimili sana magonjwa (chanjo ni Muhimu kuwapa) tofauti na kuku wa nyama au wa mayai.
Nyama yao ni nzuri sana haina tofauti na kuku wakienyeji.
Wanauzito mkubwa kuku mmoja anafika hadi kilo sita.
Soko lake ni kubwa.
KUKU WAKIENYEJI.
Hawa ni kuku ambao asili yake ni hapa hapa Tanzania na tunao katika maeneo mengi ya nchi yetu, kuku hawa wanakuwa wana maumbo madogo kulinganisha na kuku chotara, pia kuku hawa hawakui kwa haraka ukilinganisha na kuku chotara, aina hii ya kuku hutaga mayai machache sana kwa mwaka na wanataga mayai kati ya 40-120.
Faida ya kuku hawa.
Kuku hawa wanafugika katika mazingira yeyote yale kwa sababu ni wazuri kujitafutia chakula, ili upate faida nzuri ya mradi wako wa kuku huo unashauriwa kuwapa chakula cha ziada ili waweze kukua kwa haraka na kuwa na uzito mzuri.
Kuku hawa hawana gharama hivyo nashauri kama una eneo zuri ni muhimu ukaanza ufugaji wa kuku hawa kwa sababu hawana shida katika ufugaji wake.
Kuku hawa wanapendwa sana hapa nchini kwa sababu ya nyama na mayai yake kuwa mazuri sana na ni kuku wa asili hivyo tunaamini hawana kemikali na hii ni kweli kabisa,
Hizi ni aina mbalimbali za kuku katika nchi yetu na jambo la muhimu kuangalia malengo yako na uhitaji ya jamii husika jambo nzuri na lakuvutia ni kwamba aina hizi za kuku zinafugika katika maeneo yetu yote ya nchini hivyo angalia mazingira yako na anza kufanya ufugaji.