Fahamu Vyanzo vya Utajiri vya Wachungaji Wengi

 Mchungaji ni kiongozi mwenye jukumu la kuwalinda na kuwaongoza waumini wake, kwa mafundisho mbalimbali ya kiroho. Jina hili siyo geni katika masikio ya wengi.

Wachungaji jukumu lao kubwa ni kuhakikisha kuwa waumini wanapewa mafundisho ya kiroho ya namna ya kuenenda na kuishi kufuata maagizo waliyopewa na Mungu.

Katika makala hii, tunajaribu kuangalia namna ambavyo baadhi ya wachungaji hutumia njia mbali mbali kuhakikisha kuwa wanajiingizia kipato na kujipatia utajiri kupitia kanisa.

Hapa naomba ieleweke kuwa, siyo wachungaji wote wanaotumia mbinu hizi kujipatia utajiri, wapo ambao ni waaminifu na hutumia kwa kasi walichopangiwa. Lakini wapo baadhi ambao utakuta wanaishi maisha ya raha, wanafuja fedha, wanamiliki magari ya thamani, wanaishii katika nyumba za kifahari n.k. hawa ndio tunaowazungumzia hapa.

Katika kuhakikisha kuwa wanapata utajiri kutoka kwa waumini wao, hizi ni baadhi ya mbinu wanazozitumia wachungaji hao ili kujiingizia kipato cha ziada.

Uchapishaji wa vitabu

Wachungaji wengi wamekuwa na kaida ya kuandika vitabu mbalimbali vyenye mafunzo ya aina tofauti tofauti. Uuzwaji wa vitabu hivyo hufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na nguvu ya ushawishi waliyo nayo wachungaji. Hata kama kitabu hicho hakijakidhi ubora, alimradi tu kimeandikwa na mchungaji, basi waumini watashawishiwa kukinunua. Na kupitia mauzi ya vitabu hivyo, basi wachungaji hujiongezea kipato jambo ambalo huchangia wao kuwa matajiri.

DVD na CD

Kama wewe ni muumini wa dini ya kikristo, basi utakubaliana na mimi katika hili. Siku hizi katika makanisa mbalimbali kumekuwa na CD na DVD za mafundisho mbalimbali zinazouzwa. Utakuta CD ya mahubiri ya Ibada ya jumapili iliyopita, yanauzwa jumapili hii kwa waumini walewale waliokuwa wamehudhuria ibada hiyo. Kununua CD ya mafundisho ili urudie kuisikiliza mara kwa mara ni jambo jema sana. Lakini tatizo ni pale ambapo waumini wanauziwa CD hizo kwa bei ya faida. Yaani utakuta gharama za maandlizi na ya CD hizo mpaka zikamilike, ni ndogo sana kulinganisha na kiwango wananchotozwa waumini. Hii ni njia ambayo wachungaji wengi huitumia kujipatia kipato, na waumini wengi bado hawajaitambua.

Semina

Semina mbalimbali za mafundisho ya dini zimekuwa zikiandaliwa na wachungaji wengi. Kumekuwa na semina za vijana, semina za watoto, semina za wanandoa, semina za akina mama na nyingine nyingi. TAtizo siyo seina hizi, tatizo ni pale ambapo wewe kama muumini wa kanisa hilo, ili uweze kuhudhuria semina hiyo, basi inakubidi kulipia kiasi fulani cha fedha kama kiingilio.

Semina za aina hii mara nyingi hutangazwa sana na wachungaji hutumia nguvu kubwa kuwashawishi waumini wahudhurie. Sawa, kazi yao ni kuokoa roho nyingi, lakini kwa upande wa pili (kibiashara) wanapohudhuria watu wengi, ndivyo pesa nyingi ya kiingilio itakavyopatikana.

Ushawishi mkubwa kwenye utoaji wa sadaka

Kutoa ni moyo, na kadiri unavyotoa kwa wingi, ndivyo unavyopata baraka. Ni kweli, lakini wachungaji wengi hutumia mwanya huu kuwashawishi waumini wao kutoa zaidi na zaidi. Kumbuka hata maandiko ya Biblia yanasema toa kwa kadiri ya uwezo wako, siyo tu kutoa hata kama huna, na wala usitoe eti kwa sababu mchungaji amesisitiza ufanye hivyo.

“Kila mmoja na afanye kama alivyoazimia moyoni mwake, si kwa kutopenda, wala kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda mtoaji mchangamfu” 2 Wakorinto 9:7

Mishahara mikubwa

Biblia inafundisha kuwa wote wanaotoa huduma za kiroho wanapaswa kulipwa. Na malipo yao hayatoki pengine popote zaidi ya kwenye matoleo na sadaka za waumini.

Wazee wanaowaongoza watu vizuri wanastahili kupata riziki maradufu, hasa wale wanaofanya bidii katika kuhubiri na kufundisha. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Usimfunge ng’ombe kinywa anapopura nafaka.” na tena “Mfanyakazi astahili malipo yake.” 1 Timotheo 5: 17-18

Wapo viongozi wa dini ambao wanatumia sadaka za waumini kujipatia mishahara mikubwa na kuishi maisha ya starehe na ya kitajiri. Hawa wameonywa katika Biblia kuwa wasiwe na tamaa ya fedha bali waifanye kazi ya Mungu kwa kujitolea.

“wazee! Mimi niliye mzee ninalo ombi moja kwenu wazee wenzangu. Mimi mwenyewe nilishuhudia kwa macho yangu mateso ya Kristo na natumaini kuushiriki ule utukufu utakaofunuliwa. Mimi nawaombeni. mlichunge lile kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mlitunze si kwa kulazimika, bali kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo si kwa tamaa ya fedha, bali kwa moyo wenu wote. Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa hilo kundi.” 1 Petro 5: 1-3
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad