Familia ya Lissu Imelitaka Bunge Kutoa Fedha za Matibabu ya Lissu

Familia ya Lissu Imelitaka Bunge Kutoa Fedha za Matibabu ya Lissu
FAMILIA ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), imelitaka Bunge kutoa fedha za matibabu yake kama halitaki mtunga sheria wake huyo akafukuzwe hospitalini alikolazwa.


Lissu amelazwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Luvein nchini Ubelgiji tangu mapema mwezi huu baada ya kutibiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa miezi minne.

Msemaji wa familia ya Lissu, wakili Alute Mughwai, aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa miezi ni mitano sasa Lissu hajapata stahiki zake kimatibabu kama Mbunge.

“Tumemaliza miezi mitano tangu kutokea kwa tukio la kushambuliwa kwa Lissu na Bunge kama taasisi limeshindwa kutoa fedha za matibabu kwa mwenzao," alisema Mughwai.

“Sasa Lissu atalaumiwaje? Akilia Mungu wangu mbona umeniacha, Bunge langu mbona limeniacha... au wanataka afukuzwe hapo hospitalini kwa kukosa fedha za matibabu?

“Mpaka sasa hatujui kinachoendelea. Tunaweza kusema ni siasa au kwa namna nyingine tunaweza kutafsiri kuwa sababu Lissu ni mkosoaji mzuri wa serikali bungeni.

“Waheshimiwa hawa wanataka mwenzao kuwa kilema au kupoteza maisha? Cha msingi wanapaswa kutoa haki za msingi ambazo sisi tumeona zinacheleweshwa kwa makusudi.”

Bunge lilishasema hata hivyo kwamba Lissu alifuata matibabu nje ya nchi kinyume na utaratibu wa bima ya afya ya wabunge, hivyo kuwa kikwazo cha kuhudumiwa kwake.

Lissu (49) alipigwa risasi tano na watu wasiojulikana akiwa kwenye gari nyumbani kwake Area D mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana. Jumla ya risasi 32 zilirushwa na watu hao kwa mujibu wa taarifa za Bunge.

Akizungumzia mawasiliano ya familia na ofisi ya Bunge, alisema Desemba 15, mwaka jana, alitoa mrejesho kwa vyombo vya habari kuhusu barua waliyoandikiwa na Katibu wa Bunge ikiwataka familia hiyo kutoa ufafanuzi wa haki zipi ambazo Lissu anatakiwa kupewa na Bunge.

Alisema waliandika barua ya kuomba ufafanuzi huo, Desemba 13, mwaka jana, na barua hiyo ilipokelewa na Ofisi ya Bunge Desemba 18, mwaka jana na ilipokelewa kwa njia ya barua za haraka ya DHL.

“Tulichoomba ufafanuzi ni kuhusu fedha za matibabu, stahiki za usafiri wa kwenda nje ya nchi pamoja na posho ya kujikimu kwa yule anayemuangalia hospitalini," alisema.

“Bunge ilitoa majibu Desemba 10, mwaka jana, kupitia kwa Katibu wa Bunge ambapo alidai kuwa barua hiyo iliwaelekeza kurudia utaratibu wa kufuata utaratibu ambao bunge linatumia kwa ajili ya matibabu ya wabunge pindi wabunge wanapokwenda kupewa matibabu,” alisema.

Aidha alisema baada ya kurudia kufanya marekebisho ya barua hiyo, Katibu wa Bunge aliwajibu Januari 10, mwaka huu, kuwa Wizara ya Afya imeunda timu ya madaktari bingwa kwenda Nairobi kumuangalia Lissu wakati wakitambua kuwa mbunge huyo Januari 6, mwaka huu, alishasafirishwa kwenda nje ya Afrika kwa ajili ya matibabu.

Akizungumzia afya ya Lissu, Mughwai alisema kwa sasa anaendelea vizuri na mazoezi ya viungo, ili kuimarisha afya yake.

Alisema aliwasiliana na Lissu Jumapili ambapo alimweleza anaendelea vizuri na mazoezi akiwa anafanya mara tatu kwa siku.

Alisema mazoezi anayofanyishwa kwa sasa ni kupanda ngazi sita na kuvuta vitu vizito.

Aidha alidai kwa mguu ambao ulipata majeraha makubwa unaweza kustahimili kusukuma kitu chenye uzito kwa kilo 25 na kwamba mazoezi yataendelea hadi hapo atakapo kuwa vyema kiafya.

KIASI CHA FEDHAOktoba 17, mwaka jana, wakati Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuzungumzia hali ya afya ya Lissu, alisema kiasi cha fedha kilichokuwa kimepatikana hadi Oktoba 12 kutokana na michango ya wadau waliopo ughaibuni kilikuwa Dola za Marekani 29,700 (Sh. milioni 64.9).

Katika mkutano wake huo wa Oktoba 17, Mbowe alisema kuwa tangu alipolazwa Septemba 7 hadi Oktoba 12, Lissu alikuwa amefanyiwa operesheni 17 na matibabu yake yalikuwa yamegharimu Sh. milioni 412.

Katika shambulio hilo ambalo limelaaniwa na watu wengi wa ndani na nje ya nchi, akiwamo Rais John Magufuli, Lissu alivunjika mguu wa kulia, mkono wa kushoto na nyonga.

Baada ya tukio hilo, Lissu aliwahishwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma ambako alipatiwa matibabu ya awali kabla ya kusafirishwa kwenda Kenya kwa ajili ya matibabu zaidi.

Taarifa za awali zilidai watu waliompiga risasi walikuwa wakimfuatilia kutoka bungeni, na kwamba walikuwa wakitumia gari nyeupe aina ya Nissan Patrol.

Hadi sasa polisi haijamkamata mtu yeyote kuhusiana na shambulio hilo.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Nyie kweli Hamnazo.... Kwa Minajili gani na Misingi ipi ya huyu Traitor....
    Uamuzi Wenu ni lazima majuku yake mchukue.

    ReplyDelete
  2. halafu niwaulize nani aliyempeleka lisu huko na inakuaje aliyempeleka ashindwe kumlipia hizo gharama? na badala yake bunge lilaumiwe? hivi mlipokuwa mnachukuwa maamuzi tulijua mnajiweza mbona mnalia sasa? kila siku kwenye vyombo vya habari jamani tumewachoka. fikiri kabla ya kutenda

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad