Na Baraka Mbolembole
KUELEKEA mchezo wa Alhamis hii dhidi ya vinara Simba, kocha mkuu wa timu ya Singida United, Hans van der Pluijm amesema anawachukulia mabingwa hao wa zamani kama washindani wake wengine katika ligi na atakiingiza kikosi chake katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ‘tahadhari’ kubwa licha ya ukweli haihofii timu hiyo iliyofunga magoli 12 katika michezo 12 iliyopita.
“Naichukulia Simba kama timu nyingine. Siwezi kuweka akili yangu yote kwao.” Anasema Hans nilipofanya naye mahojiano Jumanne hii. Inatakiwa tuwe makini na tucheze mchezo wetu kwa kujitambua na kuimarisha morali ya timu nzima. Inatakiwa tufanye kazi yetu vizuri katika kila nafasi na katika uchezaji wa mpira pia.”
Singida wamepanda daraja msimu huu lakini namna timu hiyo inavyoendeshwa imesaidia kwa kiasi kikubwa kusajili wachezaji mahiri kutoka ndani na ng’ambo, ikiwemo kumtwaa kocha Hans ambaye aliipa Yanga mataji mawili mfululizo ya ligi kuu.
Mudathir Yahya, Ken Ally, Deus Kaseke, Kiggy Makassy, Daniel Lyanga, golikipa Peter Manyika ni baadhi ya nyota wazawa ambao wamesajiliwa na klabu msimu huu. Mzimbabwe, Tafadzwa Kutinyu, Mganda, Shafiq Batambuze, Wanyarwanda, Michael Rusheshangoga, Danny Usengimana wamefanya kikosi hicho kuwa imara na ushindi wowote utawafanya kuwa pointi sawa na Simba.
Hans ni kocha mwenye uzoefu mkubwa sasa hadi katika soka la Tanzania. Amewahi kuishinda Simba katika michezo yote miwili ya ligi kuu msimu wa 2015/16 ameendeleza aina ya soka lake la kushambulia katika kikosi cha Singida. Atawavaa Simba kwa mara ya kwanza akiwa nje ya kikosi cha Yanga huku akiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo mmoja tu vs Simba.
“Mpira hautabiriki. Kila kitu kinawezekana, Simba bado ni timu kubwa na nawaheshimu lakini siwaogopi. Tunajiandaa vizuri na timu ipo katika morali, natumaini tunaweza kuwashangaza siku ya mchezo. Hii mechi wachezaji wanatakiwa wawe makini wao wenyewe ili tupate matokeo mazuri. Ni mechi yetu muhimu.” Anasema Hans ambaye atamkosa mfungaji wake namba moja Usengimana.
Singida wamekusanya alama 23 katika michezo 12 iliyopita. Wakiwa nafasi ya nne ya msimamo pointi tatu nyuma ya Simba, timu hiyo kutoka mkoani Singida imeonyesha mwanga kuwa huenda wakawa washindani wa kweli katika mbio za ubingwa msimu huu kutokana na uimara wa timu yao.
“Njia bado ngumu, chochote kinaweza kutokea muda wowote. Tunaichukulia ligi ‘mchezo kwa mchezo’ mwishoni tutajua tulipofika. Inatakiwa tufanye kazi yetu vizuri.” Anamaliza kusema Hans.