Hatima ya Muswada umri wa Kustaafu Kujulikana J'tatu

HATIMA ya kujadiliwa au kutojadiliwa bungeni kwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 5 wa Mwaka 2017 inatarajiwa kujulikana Jumatatu, serikali itakapowasilisha majibu ya hoja za Bunge kuhusiana na muswada huo.

Huku Bunge kupitia Kamati yake ya Kudumu ya Katiba na Sheria likiufumua muswada huo kwa lengo la kuuboresha, suala la umri wa kustaafu kwa wataalamu wabobezi wakiwamo madaktari bingwa na maprofesa wa vyuo vikuu, limeibua ukinzani wa mawazo uliosababisha kamati kuitaka serikali ikajipange kujibu hoja zilizotokana nalo kufikia Jumatatu.

Kama serikali itajibu hoja hizo za kamati, muswada huo uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni wakati wa mkutano wa tisa wa Bunge 11, utajadiliwa katika mkutano unaoanza Jumanne.

Akizungumza na Nipashe jana kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa, alisema Alhamisi walipoketi kwa majadiliano, waliipa serikali hadi Jumatatu kuhakikisha inajibu hoja muhimu ambazo ziliibuka wakati wakiuchambua.

"Tumeiambia serikali kutuletea majibu ya maswali ambayo tunaamini ni lazima yajibiwe kwanza. Mfano, tunapitisha sheria hii (kuhusu umri wa kustaafu) ambayo imewatenga baadhi ya watu," Mchengerwa alisema."Ni sheria ambayo ukiiangalia katiba utafikiri ni sheria ya kibaguzi lakini tukaridhia kwa sababu ya madhumuni ya sheria yenyewe ambayo yanakwenda kutatua tatizo fulani ambalo lipo kwa kipindi kirefu.

"Mimi kwa mamlaka yangu nikatumia Ibara ya 13(5) ya katiba kuonyesha kwamba sheria hii tumeiondoa katika tafsiri ya ubaguzi kwa sababu inakwenda kutatua kero fulani na ibara hiyo inaridhia kwamba serikali inaweza kufanya hivyo kama inalenga kutatua kero fulani.

"Lakini pia sheria hii itadumu kwa kipindi gani? Maana sasa wataalamu hawatoshi. Je, wataalamu wakipatikana sheria hii itaendelea kufanya kazi? Haya ndiyo maswali ambayo tunataka yapatiwe majibu, na serikali inachukua hatua gani kudhibiti au kuongeza idadi ya watalaamu.

"Kwa hiyo tunataka serikali ituambie inachukua hatua gani wataalamu wapatikane na je, sheria hii itakaa katika nafasi gani watakapopatikana wataalamu wa kutosha? Haya ndiyo maswali ya msingi ambayo majibu yake tunatakiwa kuyapata kabla ya Jumatatu na kufanya maamuzi."

Alisema kanuni za 84 na 85 za Bunge zinampa mamlaka mwenyekiti wa kamati kuwasilisha kwanza taarifa kwa Spika kwamba amejiridhisha na muswada husika, hivyo kama wataona kuna baadhi ya mambo hayajakaa sawa, atatumia mamlaka yake hayo kumwambia Spika muswada huo usijadiliwe bungeni hadi wajiridhishe na kuona kama kila kitu kimekaa sawa.

"Kimsingi, kamati yetu imefanya kazi kwa kipindi kirefu bila kukinzana sana na serikali kwa sababu tunafanya kazi ambayo serikali inaafiki moja kwa moja kwa mambo ambayo tunayatoa," alisema.

MUSWADA WAFUMULIWA

Mbunge huyo wa Rufiji (CCM) alibainisha kuwa kwenye muswada kulikuwa na mambo ambayo hayakuwa na tafsiri na baadhi ya vifungu wameviondoa . kamati ilipata fursa Tumeuboresha sana muswada kwa nia ya kuuboresha.

Alisema kuwa miongoni mwa vifungu vilivyoondolewa ni kinachompa mamlaka waziri kushauriana na Rais kuongeza umri wa kustaafu kwa mtumishi.

"Jambo ambalo tumelikataa moja kwa moja ni kumpa mamlaka waziri. Ukisoma kifungu cha 25(A) kinampa mamlaka waziri akishauriana na Rais kuongeza umri wa kustaafu.

"Sasa sisi kama kamati tumeona kwamba hatuwezi kutoa mamlaka hayo ambayo ni makubwa sana. Kwanza ni kinyume cha katiba kwa sababu ukimpa waziri mamlaka ya kutengua kustaafu kwa mtu au kuamua wakati gani (astaafu), nadhani umenipata vizuri.

"Tukaona kwamba haya ni mamlaka makubwa sana ambayo yanaweza kuwa 'abused' sana na yakatumika vibaya."Alisema kamati yake haitoi maamuzi yenyewe tu, bali hutoa baada ya kuwaita wadau na kupata mawazo yao na kwamba katika kujadili muswada huo wapo wadau waliofika mbele yake wakiwamo watumishi wa serikali.

"Kwa hiyo tukaiagiza serikali ikiondoe kifungu kile (cha mamlaka ya waziri) kwa sababu hakina maslahi kwa taifa na pia ni kinyume cha katiba. Lakini pia ukiangalia umri wa kustaafu, tumejibizana sana na serikali," Mchengerwa alisema.

"Watu (wadau) wengi waliofika mbele ya kamati hawakuafikiana na yale maoni. Hatukuweza kupata wadau wa kutosha kwenye jambo hili nikimaanisha kwamba maprofesa wenye umri wa kukaribia kustaafu wa miaka 50, miaka 60. Tulipata wataalamu wa kariba ya kawaida. Hili likawa ni tatizo kidogo."

Alibainisha kuwa msimamo wa kamati ni kwamba umri wa kustaafu kwa hiari (kwa wataalamu wabobezi na maprofesa) ubaki ileile miaka 55 hadi 64 na ule wa lazima uwe 65, lakini wanaendelea kupata maoni mengine ya kupunguza au kuongeza ambayo yanawafanya wafikirie kubadili msimamo wao.

Alisema kuna mambo ambayo wamehitaji wayapate ili wajiridhishe zaidi kabla hawajafanya uamuzi wa kukubaliana na serikali au wabaki na msimamo wao.

"Kuna watu ambao wanasomeshwa na serikali halafu akifika miaka 55 anaomba kustaafu. Kwa kuwa serikali haina mtaalamu wa aina ile inabidi serikali ijadiliane naye, iingie mkataba naye, ni gharama kubwa sana kuingia naye mkataba," alisema.

"Kwa hiyo huyu ambaye amefikia umri wa miaka 55 ataendelea kupewa mkataba? Kama ataendelea kupewa mkataba, hakuna maana ya sheria hii.

Inamaanisha sasa ni bora tuirudishe kwenye miaka 60 mpaka miaka 65 upande wa hawa wataalamu ambao ni madaktari bingwa na maprofesa na wahadhiri waandamizi ambao wanaingia katika mfumo huu wa ajira."
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad