Jeshi la Polisi Kanda Maalum jijini Dar es salaam limetoa tathmini yake baada ya tukio la kulipuka bomba la gesi kutokea Mtwara, kwenye eneo la Buguruni.
Akizungumza na mwandishi wa www.eatv.tv Kamanda wa Polisi Kanda Maalum jijini Dar es salaam Benedict Kitalika, amesema mpaka sasa hakuna taarifa ya kifo cha mtu yeyote wala majeruhi, isipokuwa baadhi ya vibanda vya wafanya biashara kwenye eneo hilo ndio vimeteketea kwa moto.
"Kifo hakuna wala kujeruhiwa mtu hakuna, isipokuwa mabandamabanda ya wafanya biashara ndio vimeungua si unajua wale huwa wanajenga kando ya barabara, na tumekuja kugundua kwamba Dawasco wenyewe walimpa mtu contractor lakini chini ya usimamizi wao wenyewe, sasa sijui kwa nini hawakumpa ramani, lakini mpaka sasa kuko shwari na wataalam wanaendelea kuunganisha", amesema Kamanda Kitalika.
Hapo jana majira ya saa 1 usiku moto mkubwa uliwaka katika eneo la Buguruni kwa Mnyamani, baada ya mafundi wa dawasco kupasua bomba la gesi kutoka Mtwara na kuleta taharuki kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.