Jacob Zuma Ateua Tume ya Kuchunguza Ufisadi

Jacob Zuma Ateua Tume ya Kuchunguza Ufisadi
Rais Jacob Zuma ametangaza kuwa ameamua kuteua Tume ya Uchunguzi wa madai ya muda mrefu kuhusu ufisadi maarufu State Capture.

Taarifa ya Zuma kwa vyombo vya habari iliyosambazwa Jumanne jioni, ilisema Jaji Mkuu, Mogoeng Mogoeng ndiye aliteua jina la Naibu Jaji Mkuu Raymond Zondo na akampa rais ambaye alimtangaza kuongoza tume hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama Kuu ya Gauteng Kaskazini kumtaka Zuma afanye hivyo katika muda wa siku 30 kuanzia Desemba 14, 2017.

Zuma anasema wakati “ana shaka” juu ya uhalali wa maagizo ya Mahakama Kuu kwamba Jaji Mkuu Mogoeng Mogoeng amteue jaji kuongoza, ameamua kwamba uchunguzi kuhusu taifa kuwekwa mfukoni “unahitaji kutazamwa haraka”.

“Hata hivyo, nachukua hatua zaidi za ushauri juu ya uendeshwaji wa rufaa hii. Nasumbuliwa kwamba suala hili limetawala mioyo ya watu kwa muda mrefu na linahitaji kushughulikiwa haraka,” alisema rais.

Tangazo hilo limekuja wiki mbili baada ya Zuma kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Juu uliomuamuru kuteua tume. “Nimekata rufaa dhidi ya amri ambazo kwa kiasi kikubwa zimejenga mwendelezo fulani kwa Ofisi ya Rais wa Jamhuri na kwa dhati yanahitaji uhakika wa kisheria,” alisema.

Rais amesema tume itakuwa na jukumu la kufichua siyo tu mwenendo wa baadhi, lakini wote wanaoweza kuwa wamehusika kulisababisha taifa au sehemu yake liathirike kwa kudhibitiwa na nguvu zilizo nje ya serikali.

“Hakuna eneo la ufisadi au mhalifu atakayeachwa kwa namna yoyote na tume hii. Vilevile nazingatia dokezo lililoonyeshwa na Mkaguzi Mkuu wa Mali ya Umma katika ripoti yake, ambamo alilalamikia ukosefu wa raslimali za kutosha kwa ajili ya kufanya uchunguzi mpana juu ya suala hili,” alisema.

Mkaguzi Mkuu wa Mali ya Umma wa zamani Thuli Madonsela alimuelekeza Rais Zuma aunde tume ya uchunguzi katika Ripoti ya Taifa Kuwekwa Mfukoni iliyoandaliwa baada ya kuchunguza madai lukuki dhidi ya familia ya Gupta, mtoto wa rais Duduzane Zuma na watu wengi walioko karibu na mkuu wan chi.

Kisha mwanamama yule aliagiza Jaji Mkuu Mogoeng Mogoeng ateue jaji kuongoza tume kwa kuwa Rais Zuma alituhumiwa kuhusika katika mtandao huo.

Juzi Madonsela alisema ingawa anapokea uamuzi huo kwa mikono miwili, anasikitishwa kutokana na ukweli kwamba rais amechelewa sana kuchukua hatua.

Rais alitangaza uamuzi huo kupitia mkanda uliorekodiwa Jumatatu usiku, akidai kwamba anataka serikali ionekane inapambana kuondoa ufisadi.

Ukweli mara kadhaa rais amekuwa akimpinga Mkaguzi Mkuu wa Mali ya Umma na akafungua kesi mahakamani akidai iliharakishwa na mapendekezo hayakuwa ya kikatiba.

Chama cha Democratic Alliance kimepokea uamuzi huo kwa  furaha lakini kimesema umechelewa.

Aidha, DA imependekeza uchunguzi ulenge kubaini shughuli za kiuchumi za Gupta na uhusiano wao na Zuma.



Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad