Kamati Maalumu ya Kuhakiki Mali Yaanza Kuwachunguza Vigogo CCM

 Kamati Maalumu ya Kuhakiki Mali Yaanza Kuwachunguza Vigogo CCM
 Kamati maalumu ya kuhakiki mali za Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyoundwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli, imetua Arusha na kuwahoji viongozi kadhaa, wafanyabiashara na wanachama.

Kamati hiyo inayoongozwa na Dk Bashiru Ally licha ya kuhoji watu hao, pia ilitembelea baadhi ya mali za CCM mkoani Arusha.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Wakili maarufu Arbert Msando akizungumza na mwananchi jana alisema wanaendelea vizuri na kazi za kuhakiki mali za chama na uchunguzi zaidi.

“Tumewahoji baadhi ya viongozi na wanaCCM, tunaendelea vizuri, ila siwezi kusema tumebaini nini hadi sasa kwa kuwa taarifa rasmi itatolewa,” alisema Msando.

Alifafanua kuwa baada ya kukamilisha kazi hiyo, mkoani Arusha kamati hiyo, itaelekea mkoani Mwanza.

Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Elias Mpanda alithibitisha ujio wa kamati hiyo, lakini hakuwa tayari kuelezea kazi ambazo zimefanyika.

“Muda huu tupo na kamati ya kuhakiki mali za chama hivyo, siwezi kusema lolote kuhusiana na masuala ya kampeni,” alisema alipotakiwa kuelezea kampeni za chama hicho Jimbo la Longido.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha, Lengai ole Sabaya wiki iliyopita licha ya kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuunda kamati hiyo, aliomba ifike mkoani humo kwa kuwa kuna mali za chama alizodai zinatumika kwa masilahi ya wachache.

Sabaya ambaye ni diwani wa Sambasha, alisema CCM mkoani Arusha ina mali nyingi, lakini viongozi waliopita wamekuwa wakinufaika na mali hizo, kupitia mikataba mibovu na kujimilikisha baadhi ya mali.

Hata hivyo, jana alisema amefarijika kuona kamati hiyo, imetua Arusha kuanza kazi ya uhakiki na akaeleza ana imani itafanya kazi kwa uadilifu.

Hivi karibuni Rais Magufuli alikutana na kamati hiyo baada ya kuiteua na kuitaka kuhakiki mali za chama na kuhoji mtu yeyote wakiwamo viongozi na wafanyabiashara ili kuhakikisha mali za CCM zinanufaisha Wanaccm wote.

Rais Magufuli pia alitaka kamati hiyo, kupewa ushirikiano ili kuhakikisha inafanyakazi kwa ufanisi.

Kwa miaka kadhaa kumekuwapo na malalamiko miongoni mwa wanachama kuhusu kutumika vibaya baadhi ya mali za chama hicho, ikiwamo maduka, viwanja, ofisi, magari ambazo zinamilikiwa na watu binafsi.



Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad