Kauli ya Jaji Mkuu Yaamsha Upya hoja ya Mgawanyo wa Madaraka

Kauli ya hivi karibuni Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma kuwa viongozi wa Serikali na wanasiasa wasiingilie Mahakama na kudharau amri za mhimili huo, imeamsha upya hoja la mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu ya dola ambayo imekuwa mjadala kwa muda mrefu.

Mjadala kuhusu mgawanyo huo wa Serikali, Bunge na Mahakama umekuwapo nchini kwa muda mrefu hasa wakati wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba kuwa inaonekana Serikali ama inaizidi nguvu au inaingilia shughuli za mihimili mingine, licha ya kwamba yote hiyo inatakiwa kuonekana sawa.

Hata hivyo, baadhi ya watu huamini kwamba mhimili wa Serikali ambao unaongoza dolo ndio wenye nguvu kwa kuwa unasimamia mapato na matumizi ya mihimili mingine.

Hata Rais John Magufuli alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu suala hilo Novemba 2016, alisema, “Mihimili hiyo (Bunge, Serikali na Mahakama) inaweza ikalingana, lakini inawezekana kuna mhimili ambao umechimbiwa zaidi kwenda chini.”

Akisisitiza jibu lake, Rais alizungumzia jinsi alivyokwenda kwenye shughuli ya mahakama na akaombwa fedha na uongozi wa mhimili huo kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zake kwa kutambua kuwa, Rais ndiye mwenye uwezo wa kuwapatia fedha hizo.

Ndani ya mjadala huo, pia yamekuwapo madai miongoni mwa wananchi kupitia maoni yao wakati wa mchakato wa Katiba, wanasiasa, wanaharakati kuwa Serikali imekuwa inaingilia shughuli na mihimili mingine – Bunge na Mahakama, jambo ambalo linaathiri uhuru wake.

Pengine ni kutokana na madai hayo au mengine, ndipo Jaji Mkuu anaibuka na ujumbe mahususi kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa Serikali;

“Nawasihi viongozi wote wa Serikali wenye mamlaka za kikatiba na kisheria, wabaki ndani ya maeneo yao ya kikatiba na wajiepushe na kuingilia maeneo yaliyo ndani ya haki, hadhi na mamlaka ya Kikatiba ya Mahakama.”

Akaongeza kwamba kuanzia sasa (Mahakama) watakuwa wakali kwa mtu atakayeingia katika anga zao, huku akiwataka mahakimu na majaji kuchukua hatua kwa watu wanaodharau amri zao, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, mamlaka ya utoaji haki ni ya Mahakama pekee.

Hata hivyo, akijibu kwa nini aliamua kutoa kauli hiyo, Jaji Mkuu anasema ni kutokana na taarifa za vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikiripoti matukio hayo ya amri za Mahakama kuvunjwa.

Hakuishia hapo, Jaji Mkuu akawataka mahakimu ambao kwa bahati mbaya amri zao zinavunjwa na wanaonekana hawachukui hatua waanze kufanya hivyo kama Bunge linavyofanya, kwamba ukiingia katika anga zake, utaitwa mbele ya kamati, utaulizwa maswali na hatua zinachukuliwa.

Jaji Mkuu anasema Mahakama ina nguvu kama hiyo na si Jaji Mkuu mwenye nguvu hiyo pekee bali kwenye kila Mahakama; mahakama za mwanzo, mahakama za wilaya na mahakama za hakimu mkazi na asitokee mtu akajivika kofia ya kimahakama, atachukuliwa hatua.

Jaji Juma anasema kwa mujibu wa Katiba, sheria ndio inayotakiwa ipewe nguvu na si masuala ya kisiasa kwa kuwa nguvu ya Serikali ni sheria na si mtu.

“Sheria ikikupa nguvu unaitumia, ikikupa mamlaka unayatumia. Siasa haikupi nguvu, sheria ndio inakupa nguvu na tujaribu tubaki ndani ya sheria na ndani ya Katiba hakutakuwa na mvurugano. Vilevile tunawataka wale ambao wamepewa mamlaka yao, wabaki huko waliko na tukifanya hivyo hatutakuwa na migongano yoyote,” anahitimisha.

Kauli hiyo ya inaungwa mkono na Ibara ya 107 A (1) ya Katiba ya Tanzania inayosema: “Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Zanzibar, na kwa hiyo hakuna chombo cha Serikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.”

Mjadala mtandaoni

Muda mfupi baada ya maelezo hayo, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, “Mh Jaji Mkuu kauli kuhusu wanasiasa na watendaji wa Serikali kutokuingilia Mahakama ni kauli muhimu kwa wakati huu, lakini Mahakama ambayo ni imara katika haki inawezaje kukubali kuingiliwa? Mahakama inapaswa kujitazama zaidi. Mahakama ikiyumba Taifa linayumba.”

Si Lema tu aliyezungumzia hilo, wananchi wengine mbalimbali walitoa maoni yao kuhusu kauli hiyo kupitia ukurasa wa Facebook wa Mwananchi, Twitter na Instagram, huku wengine wakienda mbali zaidi kwa kumtaka Jaji Mkuu kuwaeleza maneno hayo wafuasi wa CCM, wakidai kwamba wapinzani hawana jeuri ya kuingilia Mahakama.

Kwa jinsi mjadala ulivyokwenda ni wazi kuwa Jaji Mkuu Profesa Juma ameona kuna kitu ambacho pia wananchi wanakiona hakiendi sawa na kuamua kufikisha ujumbe wake kwa njia hiyo.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanatafsiri kauli ya Jaji Mkuu kama “kuchoshwa kwa mhimili huo kuingiliwa na hivyo ameamua kufikisha ujumbe kwa wenye tabia hizo ili waache mara moja.

Hatua ya Jaji Juma bila shaka ni ya kupongezwa kwani si tu imeonyesha kwamba mahakama imezinduka na kutambua wajibu na nguvu zake na hivyo inafungua pazia la demokrasia na mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili hii mitatu ya dola.

Hatua hiyo ikizingatiwa na kutekelezwa itasaidia kuifanya mahakama iaminike na kiwe chombo pekee kimbilio kwa kila mtu kwa ajili ya utoaji haki.

Ingawa Jaji Mkuu hakutoa mifano ya matukio ya kuingilia uhuru wa mahakama, mifano ipo mingi, mfano wameshuhudiwa baadhi ya watendaji wa Serikali wakiamuru ubomoaji wa nyumba ambazo inadaiwa zimejengwa katika hifadhi ya barabara, zikiwamo zilizokuwa na amri ya mahakama ya kuzuia zisibomolewe.

Mbali na mahakama, hivi karibuni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe aliwakaririwa akisema hata Bunge limekuwa likifanya kazi kwa kuingiliwa na Serikali.

“Maneno na vitendo vya Rais vinaashiria kuwa Bunge halina uhuru wake na mimi kama mbunge nina wajibu wa kuonyesha kutopendezwa kwangu,” alisema Zitto kupitia mtandao wa Twitter na kuongeza kuwa “Ni dalili ya wazi ya kufifisha sauti ya Bunge na kupandisha sauti ya Serikali.

Moja ya matukio ambayo mbunge huyo alitaja kama kuingilia mhimili huo ni kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kwa kigezo cha gharama, huku hata vituo binafsi ambavyo vilipanga kurusha Bunge moja kwa moja bila malipo vikizuiwa.

Akijadili suala la uhuru wa mahakama na kauli ya Jaji Mkuu, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa anasema kwa muda mrefu wanasiasa na watetezi wa haki wamekuwa wakipigia kelele suala hilo lakini halikuonekana kufanyiwa kazi, hivyo hatua ya Jaji Mkuu italeta matumaini yalikuwa yametoweka.

Anasema katika suala la utoaji haki, Mahakama inapaswa kusimama kwa miguu yake isishurutishwe na isiingiliwe; majaji wazingatie sheria wakati wa kutoa hukumu.

Haiingii akilini kwamba mahakama inatoa amri fulani, lakini watendaji walioko chini ya Serikali wakapuuza na wakaendelea na shughuli zao kana kwamba hakuna amri yoyote,” anasisitiza.

“Jaji Mkuu yuko sahihi kama kweli anamaanisha. Kwa muda mrefu tumeshuhudia viongozi mbalimbali wakiwamo wakuu wa wilaya wakijitokeza kuingilia mhimili huo na kusababisha ama kupingana au kuwagawa na matokeo yake wanashurutishana na kutishana hadharani.”

Onesmo anasema hata kama Mahakama imekosea, kuna utaratibu wa kisheria wa kufuata ili kuipinga na si kama hali ilivyo sasa.

Anasema kuwa jambo hilo la kuingiliwa Mahakama likiachiwa liendelee litasababisha athari kuu tatu kwa jamii na kuzitaja kuwa ni pamoja na kuvunja Katiba.

Mosi, anasema mahakama ni chombo cha kutoa haki na endapo haitakuwa huru, ni wazi kuwa Katiba itakuwa inavunjwa na mwananchi atakosa haki zake za msingi.

Pili, anasema tatizo jingine ni kutengeneza Taifa lisilo fuata utawala wa kisheria na kwamba watu wataamua wanavyotaka wao, jambo ambalo litakuwa si zuri kwa mustakabali wa nchi.

“Jingine, ni kuingia katika migogoro isiyo na tija; itafika wakati wananchi watachoshwa na matendo hayo na kusababisha migogoro mikubwa na matokeo yake hayatakuwa mazuri,” anasisitiza Mratibu huyo wa masuala ya haki za binadamu.

Ni kutokana na umuhimu huo na mjadala mpana katika mchakato wa Katiba ikawekwa ibara ya 169 inazungumzia kwa kina uhuru wa mahakama.

Katiba inayopendekezwa

196 (1) Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, Mahakama zote zitaongozwa na masharti ya Katiba hii na hazitaingiliwa ama kwa kudhibitiwa, kushinikizwa au kupewa maelekezo na mtu au chombo chochote.

(2) Nafasi ya madaraka ya Jaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani au Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano haitafutwa wakati wowote ule ikiwa kuna mtu ambaye kwa wakati huo anashikilia nafasi hiyo.

(3) Mishahara na malipo mengine ya Majaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano yatalipwa kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina.

(4) Mshahara na malipo mengine yanayolipwa kwa Jaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani au Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano hayatabadilishwa kwa maana ya kumuondolea faida Jaji husika.

(5) Malipo ya mafao ya kustaafu ya Jaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani au Mahakamu Kuu ya Jamhuri ya Muungano hayatabadilishwa kwa maana ya kumuondolea faida Jaji husika wakati wote wa uhai wake.

(6) Jaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani, Mahakamu Kuu ya Jamhuri ya Muungano au Mahakama Kuu ya Zanzibar hatashtakiwa kwa jambo lolote alilolifanya au kutolifanya kwa nia njema katika   

Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Wanaharakati!!!???
    Kukomboa sauzi Sudani au polisario?
    Mbona mnajuvisha msivuo weza kuviva?
    Wahariri Ni lazima mpitie habari na maudhui yake.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad