Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amekipongeza kikosi maalum Kibiti kwa kazi waliyoifanya ya kulinda amani katika maeneo ya Kibiti, Rufiji, Mkuranga, na Mafia Mkoani Pwani.
Pongezi hizo zimetolewa na Kamanda Mambosasa mara baada ya kufanya ziara maalum kwenye kambi ya kikosi hicho kilichopo Wilayani Rufiji ikiwa ni sehemu ya ujirani mwema na kusema kazi inayofanywa na kikosi hicho matunda yake yanaonekana hadi nje ya mipaka ya Mkoa wa Pwani na kuwataka askari hao kuendelea kufanya kazi zao kwa weledi.
"Chini ya usimamizi wa Mkuu wa Oparesheni, Naibu Kamishna wa Polisi, Liberatus Sabas Kibiti, Rufiji hali imekuwa shwari kwani awali hali ilikuwa mbaya. Hakuna asiyejua kuwa ilifika mahali watu wakawa wamekata taamaa na hata kukimbia maeneo yao na wengine wakisema Tanzania haijawahi kupitia maisha ambayo watu walikuwa wanapitia. Tunawapongeza sana kwa kazi nzuri" amesema Mambosasa.
Katika msafara huo Kamanda Mambo sasa ameongozana na makamanda wa mikoa ya kipolisi ya Ilala, Temeke, na Kinondoni, ambao wamesisitiza ushirikiano baina ya vikosi vya ulinzi bila kujali mipaka.
Mkoa wa Pwani ulikuwa ukikabiliwa na mauaji ya viongozi wa ngazi mbalimbali na pia raia wasio na hatia, ambayo yalikuwa yakitekelezwa na watu wasiofahamika huku mara nyingi yakihusisha uvamizi kwenye nyumba za wahusika na pia matumizi ya risasi.
Kutokana na kushamiri kwa mauaji hayo na vitisho vilivyokuwa vikitolewa na wauaji, baadhi ya watendaji walilazimika kukimbia makazi yao.
Tukio la mwisho kutokea wilayani Kibiti ni la Juni 27, ambapo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangwi, Michael Nicholaus na mtendaji wa Kijiji hicho kilichoko Kata ya Mchukwi, Mwilami Shamte, waliuawa kwa kupigwa risasi na kufanya idadi ya waliokwishauawa Pwani kufikia 37.
Hata hivyo hali ya kurejesha amani wilayani humo ilitokana na juhudi za jeshi la polisi nchini, chini ya IGP Simon Sirro, ambaye mara baada ya kuteuliwa alifanikiwa kukomesha mauaji hayo na polisi ilitangaza kuwaua watuhumiwa wa mauaji 13 waliodaiwa kutekeleza mauaji Kibiti, Mkuranga na Rufiji.
Kikosi Kilichofanikisha Kurudisha Amani Kibiti Chapongezwa
0
January 03, 2018
Tags