IKIWA ni siku moja baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuvipiga faini vituo vitano vya runinga kwa kuvunja sheria za urushwaji wa matangazo na maudhui, Kituo cha Haki za Binadamu, LHRC kimeijia juu mamlaka hiyo na kusema hizo ni mbinu za serikali kukataa kukosolewa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kidjo Bisimba, alianza kwa kutoa pole kwa vituo vyote vilivyopigwa faini na kuongeza kwamba wapo kwenye mpango wa kuanzisha harambee ya kuvichangia vyombo hivyo vya habari kulipa faini.
Kuhusu makosa ambayo vituo hivyo viliyafanya, Bisimba anasema habari iliyoleta matatizo, haikuwa ya uchunguzi bali uchambuzi ambao kimsingi huwa hauhitaji mizania ya habari.