Mshambuliaji wa Mbao FC ya Mwanza, Habibu Kiyombo amechaguliwa Mchezaji Bora wa mwezi Disemba wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2017/2018.
Kiyombo ameibuka mchezaji bora baada ya kuwashinda wachezaji wenzake wawili alioingia nao fainali kutokana na tathmini iliyofanywa na kikao cha Kamati ya Tuzo wiki hii.
Kwa mwezi Disemba ambao timu 12 kati ya 16 zinazoshiriki ligi hiyo kila moja ilicheza mechi moja, Kiyombo aliisaidia timu yake kufunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Yanga ambao Mbao ilishinda mabao 2-0.
Kutokana na matokeo hayo, Mbao ilipanda kutoka nafasi ya nane hadi ya saba katika msimamo wa ligi, huku Kiyombo akifikisha mabao saba ya kufunga kwake msimu huu, akiwa nyuma ya Emmanuel Okwi wa Simba anayeongoza akiwa na mabao nane.
Kiyombo aliwashinda mshambuliaji wa Simba, John Bocco aliyefunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0 wa Simba dhidi ya Ndanda na beki Bruce Kangwa aliyeisaidia Azam katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stand United.
Katika mchezo huo wa Azam, beki huyo alifunga bao moja na kutoa pasi ya usaidizi wa bao lingine. Wachezaji wote hao hakuna aliyepata kadi.
Kutokana na ushindi huo, Kiyombo atazawadiwa tuzo, kisimbusi cha Azam na fedha taslimu sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wakuu wa Ligi hiyo, Kampuni ya Vodacom.
Wachezaji wengine ambao tayari wametwaa tuzo ya mwezi kwa msimu huu ni Emmanuel Okwi (Agosti), Shafiq Batambuze (Septemba), Obrey Chirwa (Oktoba) na Mudathir Yahya( Novemba).