Lipumba, Nchemba na Nape Wafunga Kampeni za Udiwani


Kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani utakaofanyika zimefungwa leo kwa wagombea na wapambe wao kutoa tambo mbalimbali.

Majimbo yatakayofanya uchaguzi huo kesho Januari 13, 2018 ni Longido, Singida Kaskazini, Songea Mjini pamoja na Udiwani kwenye Kata kadhaa.

Katika jimbo la Singida Kaskazini, Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Dk Mwigulu Nchemba amefunga kampeni hizo katika Kijiji cha Pohama tarafa Mgori alikozaliwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Lazaro Nyalandu.

Dk Mwigulu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani akimnadi mgombea wa CCM Justine Monko amewahimiza wapinga kura kumpingia kura Monko kama njia ya kuunga mkono kazi inayofanywa na Rais John Magufuli.

"Ndugu zangu wa Pohama na hasa marafiki wa Nyalandu (Lazaro), msinune kwa vile rafiki yenu amehama mkaacha kuipigia CCM, mpeni kura Monko kwa vile Nyalandu pengine alighafilika na akazinduka akarejea CCM ambayo wewe hukuipigia kura,” amesema Dk Mwigulu.

Dk Mwigulu ametumia mkutano huo kuwaonya wale wote watakaothubutu kuvurunga uchaguzi huo wa udiwani na Ubunge kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Akiomba kura, Monko amewaomba wananchi wa Singida Kaskazini kumchagua kwani uzoefu anao kupitia majukumu aliyonayo sasa ya Ukurugenzi wa Halmashauri ya Liwale mkoani Lindi na pindi wakimwamini kumpa jukumu la kuwawakilisha ataanza na kero za Pohama.

Naye mbunge wa zamani wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi) ambaye amehamia CCM, Moses Machali amesema  “Rais Magufuli amefilisi sera zote za upinzani na ndicho kitendo kilichotufanya sisi kuja CCM.”

“Enzi zetu sisi ndio tulikuwa wapinzani wa kweli, upinzani wa sasa umejimaliza wenyewe baada ya kuamua kwa makusudi kupokea mafisadi na ndio maana hawana nguvu,” ameongeza

Naye mbunge wa Mtama Nape Nnauye (CCM) akifunga kampeni Longido amewataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua Dk Steven Kiruswa kwani kwa sasa upinzani umekufa na waliopo wanapaswa kuondoka wasing’ang’anie huko kama kupe katika ng’ombe wasubiri hadi afe.

Huko Songea Mjini, Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasas, Profesa  Ibrahim Lipumba akifunga kampeni katika Viwanja vya Soko Kuu amewataka wananchi kuchagua mgombea wa Chama hicho Christina  Thinangwa.

Profesa LIpumba amesema endapo watamchagua mgombea wa CCM, Dk Damas Ndumbaro hawatoweza kutatua migogoro inayoendelea ndani ya Baraza la madiwani wa Manispaa ya Songea.

Amesema Thinangwa atasaidia kupunguza matatizo ya vifo vya kinamama kwani wanawake wengi  wanafariki dunia kutokana na kukosa damu, kutokuwa na uwezo wa kulipia gharama za afya iwapo watapata mtu wa kuwasemea matatizo yao yatatatuliwa na mtu pekee ni mgombea wa CUF.

Kuhusu hali ya uchumi, Profesa Lipumba amesema Tanzania haiwezi kufikia  uchumi wa kati iwapo haitaboresha sekta ya kilimo kwani Serikali imeshindwa kuwajengea uwezo wakulima ili waweze kuzalisha chakula kwa wingi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad