Mahakama Yaridhia Madaktari Kutoka Nje Waje Kesi ya IPTL

Mahakama Yaridhia Madaktari Kutoka Nje Waje Kesi ya IPTL
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeruhusu madaktari kutoka Afrika Kusini na India kuja nchini kushuhudia matibabu ya washtakiwa wawili katika kesi inayohusu fedha za escrow.

Kesi hiyo inamkabili Seth Harbinder Singh, ambaye ni mwenyekiti wa kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP) inayomiliki IPTL, na James Rugemalira, mkurugenzi wa VIP Engineering iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya kampuni hiyo ya kufua umeme.

Wawili hao ni wagonjwa na wamekuwa wakiomba kwenda kutibiwa nje au madaktari wao waje nchini wakati wakitibiwa.

Jana, hakimu mkazi mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba alikubaliana na maombi ya wawili hao baada ya Wakili Alex Balomi, anayemwakilisha Sethi, kudai kuwa wamethibitisha kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) haina uwezo wa kumfanyia upasuaji mteja wake.

Alisema MNH haiwezi kuondoa au kuweka puto lililo tumboni kwa mteja wake, hivyo kuomba  madaktari wake wa Afrika Kusini kuja nchini.

“Tumepokea maoni kutoka kwa hao madaktari wa Afrika Kusini kuwa ni lazima wawepo wakati wa upasuaji wa Sethi,” alisema wakili huyo wa utetezi.

Maombi kama hayo yalitolewa na Respicious Didas anayemwakilisha Rugemarila, aliyeiambia mahakama kuwa suala la afya ya washtakiwa ni muhimu sana na ugonjwa wa mteja wake ni bayana; kwamba ana uvimbe unaoonekana.

“Licha ya ugonjwa wa mteja wangu kuwa wazi, bado upande wa mashtaka haujachukua hatua yoyote kuhusu uvimbe huo,” alieleza Wakili Didas.

Alidai kuwa Rugemalira aliwahi kuugua saratani na kufanyiwa upasuaji mwaka 2008 na kwamba ugunduzi huo pamoja na matibabu yote, vilifanyika nchini India.

Didas alieleza kuwa matibabu na vipimo vilivyokuwa vinafanyika hapa nchini vilikuwa na matatizo na ndio maana aliamua kuanzisha kituo cha saratani nchini kwa ajili kutibu wananchi wasio na uwezo wa kwenda kutibiwa nje ya nchi, ili waweze kupata matibabu katika kituo chake.

Wakili huyo alisema anaamini mteja wake akitibiwa India ambako kuna vifaa na hivyo kuwa na uwezo wa kugundua tatizo la uvimbe alionao.

“Suala la afya ya mteja wangu linapaswa kupewa kipaumbele na ugunduzi wa ugonjwa wake ufanyike kwa kutumia madaktari wa India,” alisema.

Kutokana na maelezo ya mawakili wa utetezi, Hakimu Simba alisema mahakama inashukuru kwa kuona kuwa amri ya kutaka washtakiwa wakatibiwe iliyoitoa Januari 5, imetekelezwa.

Hakimu Simba alisema kutokana na hali hiyo, Mahakama imeona madaktari kutoka Afrika Kusini wa mshtakiwa wa kwanza, wawepo na utaratibu huohuo utumike kwa mshtakiwa wa pili.

“Magereza wawasiliane na madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili madaktari ya India wawepo wakati wa upasuaji,” alisema Hakimu Simba.

Awali upande wa mashtaka ulidai kuwa Rugemalira hana saratani na pia puto la Sethi limeisha muda wake.

Mwendesha mashitaka wa Takukuru, Leonard Swai alisema  hayo wakati akitoa taarifa baada ya kwenda gerezani kama alivyotakiwa na mahakama.

Swai alisema washitakiwa hao wameomba kuwa wakati wanapofanyiwa uchunguzi wa afya, madaktari wao kutoka nje ya nchi wawepo.

“Sethi ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hii, anaishi na puto tumboni tangu Desemba mwaka jana na limeisha muda wake,” alisema.

“Daktari wa Muhimbili walimfanyia uchunguzi na kubaini kuwa puto hilo linatakiwa kuondolewa na mshtakiwa alishirikishwa katika hatua hiyo akaomba daktari wake kutoka Afrika Kusini awepo wakati wa kufanyiwa upasuaji na kuomba muda wa kuwasiliana na daktari huyo.”

Hata hivyo, Swai alisema madaktari wa hapa nchini wapo tayari kuondoa puto hilo kama afya ya mshtakiwa itaendelea kuathirika au kuwa mbaya.

Pia alisema Rugemalira  anatibiwa na magereza pamoja na daktari anayeitwa Fred ambaye anachukua vipimo na kupeleka hospitalini kwake Sanitas na kurudisha majibu magereza.

Alidai katika majibu hayo yanaonyesha kuwa hana saratani kama alivyodai na kwamba Serikali inafuatilia afya zao kwa kuwa hakuna jambo linaloweza kuhatarisha maisha yao.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 2.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad