Majeruhi wa Lucky Vincent Wamejiunga na Shule Kuanza Kidato cha Kwanza

Wanafunzi watatu waliokuwa wakisoma katika shule ya Lucky Vincent ambao walinusurika katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Karatu Mei mwaka jana, wamejiunga na Shule ya Star High ya Arumeru kuanza kidato cha kwanza kwa ufadhili wa taasisi ya Stemm.

Watoto hao, Sadia Awadh, Wilson Tarimo na Doreen Mshana walifaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga na shule za Serikali lakini taasisi hiyo imechukua jukumu la kuwasomesha kuanzia kidato cha kwanza.

Jana, wanafunzi hao wakiwa na nyuso za furaha, walitembelea shule yao ya zamani na kukabidhiwa vyeti vya kuhitimu elimu ya msingi na mwalimu mkuu msaidizi, Longino Vincent.

“Tunawashukuru sana (Stemm) kwa moyo wao wa upendo na kuendelea kutusaidia baada ya matibabu yaliyofanyika Marekani. Sasa tumeanza safari yetu ya elimu ambayo tunaamini Mungu atatusaidia kuikamilisha,” alisema Wilson.

Sadia alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kuanza hatua yao nyingine ya masomo wakiwa hai na wenye afya.

Mwenyekiti wa Bodi ya Stemm na mwanzilishi wa taasisi hiyo, Steve Meyer alisema, “Hawa ni watoto wa kimiujiza, walinusurika katika mazingira ambayo ni Mungu ndiye anayejua. Hatuwezi kusema kwa nini hakuzuia ile ajali isitokee ila tumuachie yeye, sisi tutawasaidia katika safari yao ya elimu hadi mwisho wao.”

Alisema Jiji la Sioux katika Jimbo la Iowa, Marekani limeahidi kwamba iwapo watafanya vizuri katika masomo yao ya sekondari watapelekwa huko kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu.

Wanafunzi hao watatu walinusurika katika ajali mbaya ya basi iliyosababisha vifo vya wanafunzi wenzao 32, walimu wawili na dereva mmoja iliyotokea katika eneo la Mlima Rhotia.

Baada ya ajali hiyo, wanafunzi hao walipelekwa Marekani kwa matibabu zaidi na kurejea Agosti mwaka jana.

Katika hatua nyingine Meyer alikabidhi zaidi ya Sh 6.5 milioni kwa ajili ya kusaidia wanafunzi 14 wa shule ya Lucky Vincent ambao wazazi wao hawana uwezo kuwa kuwalipia ada.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad