Mama mmoja ambaye ni mkazi wa Kunduchi Beach jijini Dar es salaam Mtaa wa Kondo Ijumaa hii amejikuta katika wakati mgumu baada ya nyumba yake iliyopo mtaa huo plot No.239 Block B, kupigwa mnada ‘kimagumashi’ na kampuni ya udalali inayojitambulisha kwa jina la Nkaya Company Limited yenye makazi yake Namanga Kinondoni jijini Dar es salaam.
Akiongea na waandishi wa habari mama huyo aliyejitambulisha kwa jina la Zainabu J Kaswaka muda mfupi baada ya mnada huo, alisema tayari nyumba hiyo ilikuwa na zuio la mahakama mpaka pale kesi ya msingi itakapozungumza juu ya nyumba hiyo na deni analodaiwa mama huyo na benki moja kubwa nchini.
“Naomba msaada wa serikali kwenye hili sakata, hii kampuni ya udalali imekuja kuuza nyumba yangu wakati kuna zuio la mahakama, mwaka jana wakati wanataka kuuza nyumba yangu nilienda mahakamani na nikapewa zuio mpaka kesi ya msingi isikilizwe, nashangaa hawa wamekuja bila kutoa taarifa yoyote, hata kwa mwenyekiti hawakufika, wamekuja na mtu wao ambaye wanadai ni mnunuzi, wameuza nyumba yangu kwa milioni 200 wakati wao wanadai bilioni 1.6 kitu ambacho hakiwezekani,” alisema mama huyo.
Naye mwenyekiti wa mtaa huyo, Hamis Haule amesema ni kweli amesikia kuna kampuni ya udalali ya Nkaya ilifika mtaani kwake na kupiga mnada nyumba ya mama huyo bila taarifa yake.
“Hata mimi nimesikia hiyo habari na kwa kifupi siutambui huo mnada kwa sababu hawajanishirikisha, mimi nilitakiwa kuwepo katika mnada, na hii barua ambayo inadaiwa imesainiwa na mimi siitambui hata kidogo, hao watu wamefoji muhuri wangu pamoja na saini lakini hawajapita kwangu kabisa,” alisema Haule.
Baada ya sakata hilo, Bongo5 ilimtafuta Mkurugenzi wa kampuni ya udalali inayojitambulisha kwa jina la Nkaya Company Limited, Hassan Magogo na kuzungumza naye kuhusu sakata hilo.
“Ndugu mwandishi sisi tunafanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria, sisi tumepewa kazi na KCB na tumeifanya kama tulivyoambiwa, ni kweli hiyo nyumba niliwa na zuio la mahakama lakini lilishapita, na kabla ya huu mnada tumetangaza kwenye gazeti kwamba kutakuwa na mnada wa nyumba baada ya siku 21, na leo ni siku ya mnada tumefanya mnada na nyumba imeuzwa. Lakini pia hawajaambiwa wahame leo, notisi waliyopewa ni ya siku 30, ndani ya kipindi hicho wanaweza kufanya chochote kama wanaona wameonewa na baada ya hapo watahamishwa,” alisema Mkurugenzi Magogo.