Timu ya Mbeya City inayocheza ligi kuu soka Tanzania bara imefanya mabadiliko madogo kwenye benchi lake la ufundi kuelekea mchezo wake wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons.
Taarifa kutoka klabu hiyo imeeleza kuwa mabadiliko hayo yamewagusa kocha msaidizi, Mohammed Kijuso na Meneja wa timu Geoffrey Katepa.
Mohammed Kijuso ambaye aliwahi kuichezea klabu ya Simba anakwenda kuwa kocha mkuu wa timu ya vijana, huku aliyekuwa meneja wa timu Katepa akiachana na timu hiyo baada ya kumaliza mkataba wake.
“Kijuso anakwenda kuwa kocha wa timu ya vijana kazi ambayo aliifanya kwa mafanikio kabla ya kuwa kocha msaidizi sasa tunamrudisha huko, lakini Katepa aliajiriwa kwaajili ya kumsaidia kocha wa zamani Kinnah Phiri kwasababu hakuwa anajua Kiswahili ila kwasasa tuna mwalimu anayejua Kiswahili hivyo hakuna haja ya kumwongeza mkataba'', amesema Mtendaji wa timu hiyo Kimbe.
Kwasasa Mbeya City inayoshika nafasi ya 11 kwenye Ligi Kuu ikiwa na alama 12 baada ya mechi 12, itaendelea kufundishwa na kocha mkuu Ramadhani Nswanzurino akisaidiwa na kocha wa makipa Josiah Stephen.Kesho jioni Mbeya City itakuwa uwanjani kucheza na mahasimu wao wa jiji la Mbeya Tanzania Prison kwenye uwanja wa Sokoine.