Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe amefunguka na kulaani vikali kitendo alichofanya Waziri wa Mambo ya ndani pamoja na Waziri wa TAMISEMI kumpigia kampeni mgombea wa Ubunge wa CCM jimbo la Siha na kusema kauli zao zimejaa ubaguzi wa wazi wazi
Mbowe amesema hayo jana wakati akizindua kampeni za wagombea wa Ubunge na udiwani kwa tiketi ya CHADEMA katika jimbo la Siha na kudai Mawaziri hao wamekuwa wakitumia vibaya madaraka yao.
"Kaja Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba anawaambia kuwa lazima mchague CCM, anakuja Jafo Waziri wa TAMISEMI anawaambia wananchi wa Siha ili mpate maendeleo labda mumchague Mollel, huu ni ujinga mtupu. Tunapoongozwa na viongozi wa sampuli hizi, viongozi wabaguzi, viongozi waliopewa dhamana ya maisha yetu wakafikiri ni mali za baba zao na mama zao wanakuja kutuambia upumbavu watu wa Siha tunaakili, kujengwa kwa barabara si fadhila ya Rais" alisema Mbowe
Mbali na hilo Mbowe alisema kuwa katika uchaguzi huu wa sasa endapo wataona gari za Serikali zikitumika kwenye kampeni za wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zitakuwa halali yao.
"Mzee Mwambigija safari hii kama kufa tufe, safari hii kama noma na iwe noma tunaomba magari ya Serikali yatumike kwa kazi za Serikali hatutakuwa na ugomvi lakini magari ya Serikali na vyombo vya Serikali vikitumika kwenye kampeni za chama chochote ni halali yetu, kwa sababu nchi hii inaonekana siasa za kistaraabu haziwezekani" alisisitiza Mbowe