Mchezaji Kapombe Apimwe Mkojo?

Unaweza kuomba Shomari Kapombe apimwe mkojo kujaribu kubaini endapo anatumia dawa za kusisimua misuli, hiyo yote ni kwa jinsi jamaa alivyokamua katika mechi mbili zilizopita.

Ni nani anaweza kuamini kwa urahisi kwamba Kapombe alikaa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi sita? Amerejea na moto ulele aliokuwa akiuwasha tangu mwanzo.


Shomari Kapombe alianza kwenye kikosi cha kwanza cha Simba kwa mara ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya Majimaji tangu aliporejea kutoka kwenye majeraha ya muda mrefu.

Beki huyo ambaye amerejea Simba akitokea Azam, alipata majeraha Julai 15, 2017 akiwa kwenye majukumu ya kitaifa wakati Taifa Stars ikicheza mchezo wa awali dhidi ya Rwanda kuwania kucheza fainali za CHAN ambazo kwa sasa zinaendelea nchini Morocco.

Ni mechi yake ya pili tangu msimu huu akiwa na Simba, mechi yake ya kwanza msimu huu ilikuwa Januari 22, 2018 alipoingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Nicholas Gyan. Katika mchezo huo ambao Simba ilicheza Kaitaba dhidi ya Kagera Sugar na kushinda 2-0 Kapombe alitoa assist kwa Bocco ambaye alifunga goli la pili.

Kapombe amerudi kwa kasi na kucheza kwa kiwango cha juu katika mechi mbili alizocheza akitokea kuuguza majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa takribani miezi sita.

“Kapombe akiwa fit katika utimamu wake wa mwili ni miongoni mwa mabeki bora hapa nchini, inaonekana Simba walikuwa wakihitaji sana huduma yake kwa namna anavyocheza hasa kwa falsafa yao ya kucheza kwa kumiliki mpira wakati wote,” anasema Edgar Kibwana mchambuzi wa michezo kutoka Clouds Media Group.

Hii ni mara ya pili kwa Kapombe kutoka kwenye majeraha ya muda mrefu na kurejea kwenye kiwango kilekile, awali alikuwa Azam baada ya kukaa nje akiuguza maradhi ya tumbo, ni wachache waliamini ataweza kurudi kwenye ubora wake kutokana na kuongezeka uzito lakini mwisho wa siku alichokifanya kimebaki kuwa historia.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad